Na Veronica Simba - Nzega
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ameliagiza 
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwachukulia hatua kali ikiwemo 
kuwafikisha Mahakamani wadaiwa wake sugu hususan Kampuni na watu 
binafsi.
Dkt Kalemani alitoa agizo hilo jana wilayani Nzega, akiwa katika ziara ya 
kikazi Mkoani Tabora kukagua miradi mbalimbali ya sekta za nishati na 
madini inayotekelezwa chini ya Wizara yake.
Alisema, Serikali ilikwishaanza kulipa madeni yake kwa TANESCO, hivyo 
hakuna budi Kampuni na watu binafsi wanaodaiwa na Shirika hilo kulipa 
madeni yao pia.
“Meneja wa TANESCO, Sheria ya Umeme inakuruhusu kuwachukulia 
hatua wadaiwa waliogoma kulipa madeni yao. Wapeleke Mahakamani.”
Katika kuhakikisha agizo lake linapewa uzito unaostahili, Naibu Waziri 
aliwaagiza Mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Tabora kumpatia orodha 
ya majina ya wale wote wanaodaiwa na Shirika hilo mkoani humo ifikapo 
kesho Ijumaa, Februari 19 mwaka huu.
“Mnipatie orodha hiyo ifikapo Ijumaa, iwe ni kampuni ya mtu mzito au mtu 
mwingine yeyote,” alisisitiza. Aliongeza kuwa, ni lazima hatua stahiki 
zichukuliwe dhidi ya waliokaidi kulipa kwani kitendo hicho ni kuihujumu 
TANESCO.
Naibu Waziri alisema Serikali imedhamiria kukusanya mapato yote stahiki 
kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo alimwambia 
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora kuwa asipochukua hatua kama 
alivyomwagiza, hatasita kumuwajibisha yeye mwenyewe.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani ameagiza kuwa 
Makandarasi wote wanaojihusisha na shughuli za kutandaza waya na vifaa 
vingine kwa ajili ya kuunganisha umeme majumbani na katika majengo 
mbalimbali (wiring), kujisajili katika Ofisi za Wilaya za TANESCO.
Alisema, agizo hilo linafuatia kuwepo na wimbi la matapeli maarufu kama 
vishoka ambao hufanya kazi hiyo ya kuunganisha umeme pasipo kuwa na 
utaalam husika.
Aidha, aliwataka wananchi kutofautisha kazi zinazofanywa na TANESCO 
na zile zinazofanywa na Makandarasi binafsi katika zoezi zima la 
kuunganisha umeme.
Alisema, kazi ya TANESCO ni kusimika nguzo za umeme na kuunganisha 
Waya unaoingiza umeme katika nyumba au jengo husika lakini si kazi ya 
Shirika hilo kufunga Waya na Vifaa vya umeme ndani ya nyumba au jengo.
“Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika sana kwamba wanatapeliwa 
kwa kutozwa fedha nyingi na/au kufungiwa vifaa vya umeme visivyo na 
ubora kwenye nyumba zao. Mara nyingi lawama hizo huelekezwa 
TANESCO.”
Dkt Kalemani alisema, ndiyo maana Serikali kupitia Wizara yake, imeamua 
kuwa Makandarasi wote wanaojihusisha na shughuli hizo wasajiliwe katika 
Ofisi za TANESCO za Wilaya ili wafahamike na hivyo kuwaepushia 
wananchi adha ya kutapeliwa.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ishihimulwa, Kata ya Bukumbi, wilaya ya Nzega hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora.
Nyaya za umeme katika Kijiji cha Mambali, Wilaya ya Nzega. Kijiji hiki ni miongoni mwa vijiji vilivyounganishiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Awamu ya Pili ya REA.
 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment