HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 23, 2016

BENKI M YAZINDUA HUDUMA YA “MONEY MOJA KWA MOJA”

Katika kuendeleza utamaduni wake wa kuendana na wakati kwa kutoa huduma za kiwango cha juu, Benki M imezindua huduma mpya inayojulikana kama Money.Moja Kwa Moja ambayo itakuwa ikitumiwa na wateja wake kutuma hundi kwenda benki kutoka mahali walipo bila wao kwenda benki. Huduma hii ni ya kipekee kabisa kutokea barani Africa.

Akiongea katika uzinduzi wa huduma hiyo, naibu mkurugenzi mkuu wa benki hiyo Bi. Jacqueline Woiso alieleza kuwa katika huduma hii wateja hawatahitaji kwenda benki kwa lengo la kuweka hundi zinazotoka katika mabenki mengine. “Huduma itahusu hundi zile ambazo wateja wetu wamelipwa na wateja wao kutoka benki zingine ambao huzileta kwetu kwa ajili ya kupelekwa kwenye benki hizo ili ziweze kulipwa”, alisema.

Hii imekuja baada ya Benki kuu ya Tanzania kuboresha mfumo wa malipo kwa njia ya hundi za ndani kwa lengo la kuufanya mfumo huo kuwa salama zaidi na wa haraka, mfumo huo mpya unajulikana kwa jina la TACH na umeanza kufanya kazi hivi karibuni.

“Kupitia huduma hii ya Money.Moja Kwa Moja wateja wataepukana na foleni za barabarani pindi watakapokuwa wakielekea kwenye matawi yetu, watapunguza mahitaji ya nguvu kazi na pia hawatakuwa na haja ya kuharakisha kuwahi benki pindi muda wa benki kufungwa unapokaribia. Wateja wetu wataweza kufanya miamala ya hundi wakati wowote watakaopenda na mahali popote na kuzituma kupitia mtandao na fedha hizo zitaingizwa kwenye akaunti zao bila wasiwasi wowote. Hivyo huduma hii itawawezesha wateja wetu kupata huduma ya kibenki mahali popote walipo” alieleza Jaqueline.

“Money.Moja Kwa Moja ni huduma yenye usalama zaidi inayotumia mtandao wa intaneti ambapo mteja wetu ataweza kuweka hundi kwenye akaunti yake kwa kutumia kifaa maalum kitakachochukua taswira ya hundi hiyo na kuituma benki na pia kuihifadhi taswira hiyo endapo itahitajika baadaye. Yote haya yatafanyika hapohapo ulipo bila wewe kutoka kwenda benki”, aliendelea Bi Woiso.

Benki M ilianzishwa mnamo mwaka 2007 kwa lengo la kutoa huduma ya kiwango cha juu hapa Afrika kwa kupitia huduma zake mbalimbali. Imekuwa ni benki ya kwanza kutoa huduma masaa 12 kila siku kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa mbili usiku, siku 7 za wiki yaani Jumapili hadi Jumapili. “Pia tunatoa Garantii endapo tutazidisha muda tuliokubaliana kufanikisha miamala ya wateja, huduma hii inajulikana kama SSG (Service Standard Guarantee), huduma ambayo mpaka sasa hamna benki ingine imeweza kuwa nayo hapa nchini” alimalizia.
Mkuu wa bidhaa wa Benki M, Johnbrighton Ngowi akifafanulia jambo kwa waandishi wa habari kuhusu huduma mpya iliyozinduliwa na Benki hiyo ijulikanayo kama “Money.Moja Kwa Moja”ambayo itatumiwa na wateja wa benki hiyo kuweka taswira ya hundi na kuituma benki kutoka mahali popote walipo bila ya kwenda benki, uzinduzi huo ulifanyika jijini dare s salaam hivi karibuni. Mwingine ni naibu mkurugenzi mkuu wa benki hiyo Bi. Jacqueline Woiso.
Baadhi ya wageni waalikwa walikohudhuria uzinduzi wa huduma mpya ya benki M ijulikanayo kama “Money.Moja Kwa Moja” ambayo itamwezesha mteja wa Benki M kuweka taswira ya hundi na kuituma benki kutoka mahali popote walipo bila ya kwenda benki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad