HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 16, 2016

MAOFISA UGANI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA KILIMO

Mkuu wa wilaya ya Babati Crispine Meela

Na Woinde Shizza,Babati

Maofisa ugani na makampuni ya usambazaji wa pembejeo Wilayani Babati mkoani Manyara, wametakiwa kuwaelimisha wakulima aina ya mbegu na mbolea bora zinazofaa kulingana na udongo wa eneo husika na kuachana na kilimo cha mazoea.

Mkuu wa wilaya ya Babati Crispine Meela aliyasema hayo katika kikao cha kamati ya pembejeo kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa pembejeo kwa mwaka 2015/2016 na changamoto za utekelezaji huo.

Alisema kumekuwepo na dhana potofu kwa baadhi ya wakulima ya matumizi ya mbolea katika ardhi kuwa yanaharibu udongo na mbegu mpya zisizozoeleka kwa wakulima hazifai kutumika hivyo wataalamu wakitoa shamba darasa watawaelimisha wakulima ipasavyo.

“Suala la pembejeo ni suala nyeti kwani ni mpango wa serikali wa usambazaji wa ruzuku za vocha za pembejeo kwa wakulima na pia kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu hivyo tunapaswa kuwa makini katika hilo,” alisema Meela.

Alisema wilaya hiyo imepokea vocha za sh1 milioni 1 ambapo makampuni ya usambazaji wa pembejeo hizo kwa kupitia mawakala wao watawasambazia wakulima wa maeneo husika na kuwawezesha kupata aina zote tatu za mbegu, mbolea ya kupandia na kukuzia kwa wakati mmoja.

Alikemea baadhi ya makampuni kupitia mawakala wa usambazaji wasio waaaminifu wanaoendelea kutoa aina moja ya mbegu na makampuni hayo yazingatie sheria na kanuni za mkataba waliowekeana na halmashauri, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati Hassan Lugendo alitaka zoezi la usambazaji wa pembejeo kuharakishwa kuwafikia wakulima kwa wakati ili kuepuka malalamiko ya ucheleweshaji wa ruzuku za vocha hizo.

Ofisa kilimo, umwagiliaji na ushirika wa mji wa Babati, Daniel Luther alisema kati ya aina ya vocha 3,000 zilizotolewa ni vocha 821 pekee zimekwishapatiwa wakulima kutokana na changamoto za wakulima kupendelea kuchukua mbegu bila mbolea.

Luther alitaja sababu nyingine zilizosababisha kutochukuliwa vocha nyingi ni kuchelewa kuanza kwa msimu wa kilimo katika maeneo mengi na uelewa mdogo wa wakulima katika kutumia aina mpya ya mbegu na mbolea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad