Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuendesha kikao cha 9 cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kesho jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kitaangalia jinsi ya kutekeleza kwa haraka maazimio ya mkutano wa 8 wa baraza hilo hasa katika kuimarisha mazingira ya biashara na kujenga sekta bora zaidi ya utalii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na TNBC, mkutano huo utahusisha mawaziri, makatibu wakuu, wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali.
“Mkutano huu utaangalia njia na suluhisho madhubuti za kuimarisha mazingira ya biashara kama kurahisisha njia za udhibiti na kutumia intaneti kutoa huduma za kiserikali na biashara,” ilisomeka taarifa hiyo.
Mkutano huo utazingatia mafunzo na uzoefu wa mikutano iliyopita.
TNBC chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete ni chombo kinachotoa mwanya kwa sekta binafsi na umma kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuifanya Tanzania kuwa sehemu bora ya kufanya biashara na hivyo kuimarisha uchumi.
TNBC pia inaendesha mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya nchini yanayosimamiwa na wakuu wa mikoa na wilaya husika.
“Tangu kuanza kuongoza chombo hiki kama Mwenyekiti Desemba 2005, Rais Kikwete amefanikiwa kusaidia Baraza kufikia malengo yake kwa kiwango kikubwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, jambo hilo limeifanya TNBC kuwa uwanja maalum nchini wa kuibua mijadala ya kisera, tafiti na ushauri kwa sekta za umma na binafsi.
Mkutano wa mwisho wa TNBC ulifanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita.


No comments:
Post a Comment