Mratibu wa Kituo cha Mabinti centre cha mikocheni jijini Dar es Salaam Bi. Katia Geurts(kulia) akimwelezea jambo Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia(katikati) na waandishi wa habari jinsi kazi za ushonaji zinazofanywa na baadhi ya wakina mama waliotibiwa na kupona fistula wakati walipotembelea kituo hicho na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.
Mmoja wasichana wa kituo cha Mabinti Centre cha mikocheni jijini Dar es Salaam aliyepata kutibiwa Fistula, Happiness Christopher(kushoto)akimsikiliza Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts wapili toka kushoto akimuonesha nguo anayoendelea kuishona binti huyo wakati walipotembelea kituo hicho na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.
Mkuu wa kitengo cha Uhusiano
na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia(kushoto)akichagua moja ya
begi lililoshonwa na wakina mama wa kituo cha Mabinti centre kilichopo mikocheni
jijini Dar es Salaam wakati alipowatembelea kituoni hapo na kujionea miradi mbalimbalia inayofadhiliwa
na Vodacom Foundation,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada
ya matibabu katika Hospital ya CCBRT na kupona
ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.Kulia ni Cherry
David.
Wanawake waliotibiwa na hatimaye kupona fistula katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar
es Salaam wameamua kujikita katika sanaa ya kazi za mikono kwa lengo la
kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini.
Takribani wanawake wapatao 81, chini ya mpango
madhubuti ulioratibiwa na hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo
mbalimbali ya kazi za mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina
tofauti, utengenezaji wa mabegi, kofia, ususi na kadhalika, katika Kituo kinachoendeshwa
na hospitali hiyo kijulikanacho kama ‘Mabinti centre’ tangu mwaka 2007.
Akizungumza mbele ya ujumbe wa wadhamini
waliotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, Mratibu wa
Kituo hicho, Katia Geurts, alisema kituo hicho kinatoa mafunzo mahususi kwa wakinamama
waliopona baada ya kusumbuliwa na fistula.
“Wengi wao wanatoka katika familia duni, hivyo
mafunzo haya wanayoyapata baada ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda
kuwasaidia kujiajiri wao wenyewe jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa
maisha,” alisema Geurts.
Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo
kituo hicho huwapatia vyeti vya uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea
kazi vinavyoendana na stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya
kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.
Nae Mkufunzi wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja
wa waathirika wa ugonjwa wa fistula hospitalini hapo, Jane Rugalabamu, alisema
katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo
amebaini kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii
lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kufisha aibu.
“Kuna haja kubwa ya kuelimisha akinababa
wawaruhusu wake zao wenye matatizo waje kutibiwa. Fistula ni hali inayotibika
na wala sio hali ya kurogwa kama wengi
wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti tulikuwa na hali hiyo na
sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni,” alisema Rugalabamu.
Kwa upande wake Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa
Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia, baada
ya kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo, alisema
kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom na Vodafone duniani kote, wataendelea
kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na hali hiyo ya fistula hatua kwa hatua,
sanjari na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni inayoendelea dhidi ya hali
hiyo.
“Tutaendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa
fistula kuanzia hatua ya kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia
fedha kupitia huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu
na baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea
ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao,” alisema Mworia.




No comments:
Post a Comment