Na Magreth Kinabo –maelezo
30/09/2015
Serikali imemtaka kila mwanajamii kutafakari haki ambazo wazee wanastahili na kuweka mipango ya makusudi katika kuwawezesha kuzipata haki hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt, Donan Mmbando (Pichani) kupitia tamko la wizara hiyo kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wazee duniani itakayofanyika kesho Oktoba Mosi ,mwaka huu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu Kuwashirikisha Wazee Kwa Ustawi Endelevu Mijini”
“Uko umuhimu kwa jamii yetu kutafakari iwapo tunatambua mahitaji halisi na kuthamini michango yao kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa.
“Tunawashirikisha, tunawaheshimu na kuwaendeleza kama wananchi wengine na tunaheshimu mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee hao,” alisema Dkt. Mmbando.
Ameongeza kwamba wazee katika nchi yetu wanayo nafasi kubwa katika juhudi za kuleta maendeleo. Katika maisha ya kila siku ya jamii, wazee wanakubalika kuwa ni watoa habari, ujuzi wa mila na desturi, washauri na wapatanishi. Pia wazee ni walezi wa watoto wadogo,hususan kwa watoto yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na janga la UKIMWI.
“ Natoa wito kwa watendaji wote kwa nafasi zao mbalimbali hususan wakurugenzi watendaji Halimashauri za Miji/Manispaa/Wilaya na wakala mbalimbali zinazotoa huduma kwa wazee ili ziweke mipango inayozingatia haki za wazee na kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii iliyopo ili kuboresha huduma wanayopata,” alisisitiza.
Aidha Dkt. Mmbando alisema alisema suala la wazee ni mtambuka, hivyo kila idara na asasi mbalimbali za Serikali na watu binafsi zishiriki katika kuhakikisha kwamba juhudi juhudi za makusudi zinafanywa ili kuboresha maisha ya wazee.
Alisema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini michango inayotolewa na wazee katika maendeleo ya taifa letu.
“ Hivyo nawaomba wazee waendelee kushirikiana na Serikali yao katika kuendeleza utulivu na amani tuliyonayo na pia waendelee kuwa kielelezo bora na urithi kwa vijana wetu kwa manufaa ya taifa letu,” alisema.
Alitoa changamoto kwa vijana kuwa karibu na wazee ili kujifunza maadili mema toka kwao na kuwajibika kuwahudumia ipasavyo na kuweka taratibu za kujiwekea akiba kila wanavyopata ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufanya maandalizi ya maisha kuelekea uzeeni.
No comments:
Post a Comment