HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 28, 2015

REA KUHUSISHA SEKTA BINAFSI PAMOJA NA BENKI NCHINI ILI KUONGEZA KASI YA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI

Na Benedict John-MAELEZO-Dar es salaam
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeadhimia kuhusisha Sekta binafsi pamoja na benki nchini ili kuongeza kasi ya usambazaji umeme Vijijini.

Hatua hiyo itasaidia kuleta maendeleo ya haraka na kufikisha umeme katika maeneo ya vijijini katika maeneo mengi hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava wakati akiongea katika kikao kilichohusisha Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, sekta binafsi pamoja na benki zilizopo nchini.

Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini , kasi ya upelekaji umeme vijijini hapa nchini imeogezeka. 

“Baada ya hiki chombo kuingia kazini kasi imeongezeka kwani kwa sasa wananchi waliofungiwa umeme ni zaidi ya asilimia 24 na wakati ule namba ya uwepo wa umeme vijijini ilikuwa asilimia 10 mwaka 2005 ambapo kwa sasa ni karibu asilimia 40 na tunatarajia kuongeza kasi hii kadri tunavyozidi kupata vyanzo vingi vya fedha kwani malengo yetu hapo baadaye ni kuweza kufikia asilimia zaidi ya 70”, alisema Mhandisi Mwihava.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Dkt. Lutengano Mwakahesya ameeleza kuwa kikao hicho kinalenga  kufafanua namna gani sekta binafsi zinavyoweza kupata faida kwa kuingia katika sekta ya nishati pamoja na kushirikia katika kuleta maendeleo ya haraka katika kufikisha umeme kwa asilimia 60 na zaidi.

Amesema kuwa endapo umeme nchini utaenea katika maeneo ya vijijini utaweza kuleta maendeleo makubwa hususani katika kuleta ajira kwa vijana na kuibua miradi mbalimbali kupitia viwanda vidogo vidogo jambo ambalo litapunguza tabia ya baadhi ya watu kukimbilia mijini katika kusaka ajira.

“Maendeleo makubwa yatapatikana iwapo umeme huu utafika vijijini, utasaidia kuleta viwanda vido vidogo kama vile mashine za kukoboa ili ipatikane ajira vijijini na watu waache kuhamia mjini nkutafuta maisha bora kwanbi umeme huu utasaidia wawananchi kuibua miradi mizuri ya maendeleo”. Alisema Mwakahesya.

Ameongeza kuwa, watu wengi hawawezi kulipa shilingi 27,000 hivyo Bodi hiyo inatazamia kuongea na benki za zilizopo nchini pamoja na sekta binafsi ili kuweza kupata njia bora zaidi za kufikisha umeme katika maeneo hayo ya vijijini kwa kuwapa mkopo ambao unaweza kulipwa pole pole kwa kutumia kulipia bili za umeme.

Serikali ilikamilisha mchakato wa uanzishwaji wa Taasisi ya Wakala wa Nishati Vijijini mnamo mwaka 2005 ambapo mwaka 2007 hadi hivi sasa baada ya Wakala kuingia kazini, kasi ya upelekaji ya umeme vijijini imekuwa kubwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya wadau wa Sekta binafsi pamoja na benki zilizopo nchini wakati wa kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) juu ya kuleta maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini .
Baadhi ya wadau wa Sekta binafsi pamoja na benki zilizopo nchini wakifuatilia ajenda wakati wa kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) juu ya kuleta maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini .
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad