HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 28, 2015

WASANII WATAKIWA KUTOA ELIMU YA UPIGAJI KURA

Na Mwandishi Wetu

Wasanii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili watambue umuhimu wa kupiga kura na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa  (BASATA) Godfrey Mngereza wakati akichangia mada kuhusu Umuhimu wa Jamii kupiga kura kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

“Kama taifa tunazungukwa na matukio mengi yanayohitaji wananchi kupiga kura katika kuamua. Tuna tukio la kupiga kura ya maoni juu ya katiba inayopendekezwa lakini pia uchaguzi mkuu. Wasanii tuna wajibu wa kuwajengea hamasa wananchi kushiriki matukio haya muhimu” alisisitiza.

 Aliongeza kwamba wasanii hawana budi kutambua kwamba wana nafasi kubwa kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu nafasi waliyonayo katika kuamua hatma yao lakini pia kuwa katikati katika kuibua masuala mbalimbali yaliyoko katika jamii ili kuwapa wananchi uchaguzi sahihi linapokuja suala la kupiga kura.

“Wasanii hampaswi kuwa na upande mnapotoa elimu bali wajibu wenu ni kuibua na kuielimisha jamii kuhusu upigaji kura. Suala la nani apigiwe kura na wananchi linabaki kuwa mikononi mwa mwananchi mwenyewe ambaye ndiye mpiga kura” aliongeza.

Awali, wakitoa burudani kwenye Jukwaa hilo la Sanaa, wasanii kutoka kundi la Bongo Artists Foundation linaloongozwa na msanii wa maigizo Christian Kauzeni walitoa elimu mbalimbali kuhusu umuhimu wa wananchi kupiga kura huku wasanii hao wakionesha kwa hisia kali madhara yatokanayo na wananchi kutokupiga kura.

Kundi hilo lililovuta hisia za wadau takribani themanini waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa lilionesha madhara ya kutokupiga kura kuwa ni pamoja kupatikana kwa viongozi wabovu wasiyowajibika,kukosekana kwa huduma muhimu za jamii na changamoto nyingine nyingi ambazo zinakwamisha jitihada za wananchi kujikwamua kutoka kwenye ufukara.
Kiongozi wa Kundi la Bongo Artists Christian Kauzeni (Katikati) akizungumza na wadau wa Jukwaa la Sanaa (hawako pichani) wakati Kundi lake lilipotoa elimu kupitia Sanaa za Majukwaani kuhusu umuhimu wa wananchi kupiga kura mapema wiki hii. Kulia ni Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristide Kwizela na Afisa Sanaa wa baraza hilo Ernest Biseko.
Moja ya wasanii wa Bongo Artists akiwauliza swali la Je kutokupiga kura ni uhayawani? Wadau wa Jukwaa la Sanaa wanaomtazama. Msanii huyu alikuwa kivutio kikubwa hasa kwa kuuliza swali hilo la Je Huu ni Uhayawani? Ambalo lilienda sambamba na maudhui ya igizo la kundi hilo.
Msanii wa kundi la Bongo Artist aliyepuuza zoezi la kuwachagua viongozi akilia kwa uchungu baada ya kupata taarifa za ndugu yake kufariki Dunia kutokana na kukosa tiba na dawa kwenye hospitali aliyokuwa akitibiwa. Mama huyu alivuta hisia za watu wengi.
Kikundi cha Ngoma kutoka Bongo Artist kikionesha burudani kwenye Jukwaa la Sanaa.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza akikipongeza kikundi cha Bongo Artist kutokana na kutoa elimu ya upigaji kura kupitia sanaa za maonesho kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad