Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Petrogas inayojihusisha na kutoa mafunzo kwa ajili ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi pamoja na usimamizi wake yenye makazi yake jijini Dar es Salaam Bw. Greyson Kiondo akisisitiza jambo kwenye mafunzo yanayohusu uandaaji wa mapendekezo ya miradi na usimamizi wake yaliyoshirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini yanayoendelea mjini Bagamoyo katika hoteli ya Stella Maris.
Msimamizi wa mradi unaohusika na kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji (CADESE; Capacity Development in the Energy Sector & Extractive Industries) Bw. Paul Kiwele (kulia) akisisitiza jambo kwenye mafunzo hayo. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga.
Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga ( wa kwanza kulia mbele ), msimamizi wa mradi wa CADESE Bw. Paul Kiwele (katikati) na baadhi ya washiriki wakiendelea kufuatilia mada iliyokuwa inawasilishwa na mtaalamu mwelekezi Bw. Tom Mitro kutoka Petrogas (hayupo pichani).
Mtaaalamu kutoka Petrogas Bw. Tom Mitro akiwasilisha mada juu ya uandaaji wa mapendekeo ya miradi katika semina hiyo mbele ya washiriki (hawapo pichani).
Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli Mhandisi Hosea Mbise kwenye mafunzo hayo. Kulia ni msimamizi wa mradi wa CADESE Bw. Paul Kiwele.
Na Greyson Mwase, Bagamoyo
Waatalamu kutoka katika Sekta za Nishati na Madini nchini wametakiwa kuwa wabunifu katika maandalizi na usimamizi wa miradi ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga kwa niaba ya Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli Mhandisi Hosea Mbise alipokuwa akifungua mafunzo ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi, sera na mbinu za usimamizi wa miradi yaliyoshirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC) yanayoendelea mjini Bagamoyo.
Mafunzo haya yanatolewa na mtaalamu mwelekezi ambaye ni kampuni ya Petrogas yenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Luoga alisema kuwa Serikali imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali katika usimamizi wa miradi yake ya maendeleo, hivyo ni vyema wataalamu hao mara baada ya kumaliza mafunzo hayo wakawa wabunifu kiasi cha kuweza kuandaa mapendekezo ya miradi yanayotekelezeka, huku yakiendana na kiasi cha bajeti iliyotengwa.
“ Kama Wizara tuna kazi nyingi zinazotakiwa kutekelezwa ambazo zinahitaji uandaaji makini wa mapendezo ya miradi ( “project proposals”) ambazo zinahitaji utaalamu wa hali ya juu kuanzia uanzilishi wa miradi, utekelezaji wake na tathmini yake kulingana na kiasi cha fedha kilichotengwa, hivyo lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta za nishati na madini.” Alisema Mhandisi Luoga.
Wakati huo huo msimamizi wa mradi unaohusika na kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji (CADESE; Capacity Development in the Energy Sector & Extractive Industries) Bw. Paul Kiwele alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta za nishati na madini katika uandaaji wa mapendekezo ya miradi mbalimbali ( project proposals) na sera na hivyo kuepusha gharama ya kutumia wataalamu kutoka nje na kukuza umiliki.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatakayochukua wiki tatu yatashirikisha washiriki 60 ambapo kila kundi la washiriki 20 litajifunza kwa muda wa wiki moja, na kuongeza kuwa kundi la kwanza litajifunza juu ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi na kufanya tathmini yake ( project proposals preparations and evaluations ), kundi la pili litajifunza juu ya uandaaji wa sera na kundi la tatu litajifunza juu ya usimamizi wa miradi.
Akizungumzia uanzishwaji wa mradi wa CADESE, Bw. Kiwele alisema kuwa mradi huo ulizinduliwa mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Phillipe Poinsot.
Alisema mradi huu unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) na unatekelezwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uogozi na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

No comments:
Post a Comment