HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 15, 2014

KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI AJIONEA UHARIBIFU MKUBWA WA MABOMBA JANGWANI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Bashir Mrindoko leo ametembelea eneo la Jangwani, Darajani, barabara ya Morogoro kujionea uharibifu mkubwa wa mabomba ya maji.

Mabomba hayo ya inchi 16 yenye urefu wa mita 12 yamezolewa na maji kutokana na athari iliyoletwa na mvua kubwa ya mwishoni mwa wiki inayoendelea jijini Dar es Salaam.

“Ni athari kubwa ambayo imesababishwa na mvua hii na mpaka kukata mabomba ya maji, ni muda mrefu tangu mvua ya aina huu kutokea Dar es Salaam”, alisema Inj. Mrindoko.

“Nimekuja kuangalia hali halisi na kuona namna gani tutafanya kufanya ukarabati wa mabomba haya, ili kurudisha huduma ya maji kwa maeneo yaliyoathirika baada ya tukio hili. Tumefanya tathmini na kuona nini cha kufanya na utekelezaji utaanza mara moja”, aliongeza Inj. Mrindoko.

Uharibifu huu umeleta athari kwa maeneo ya Muhimbili, TBL, Mchikichini, Upanga na Kariakoo na katikati ya Jiji kukosa maji.

Maeneo mengine yaliyoathirika ni Mtoni kwenye mtambo wa maji, ambapo pampu za kusukuma maji kwenye chanzo cha maji zimefunikwa na maji.

Pia, Mtambo wa Ruvu Juu, Mlandizi kipande cha bomba la inchi 4 la kupoza pampu za maji ghafi cha urefu wa mita 18 kimekatika.

Hii imesababisha maeneo ya Temeke, Tandika, Mtoni, Kurasini, Wailes na Mbagala wanaohudumiwa na mtambo huo kukosa huduma, kutokana na uzalishaji kusimama.

Vile vile, mfumo wa kupooza pampu za kusukuma maji ghafi kuathirika hivyo kukosekana kwa uzalishaji tangu jana saa 11.30 jioni.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu aliongozana na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Jackson Midala, Inj. Pascal Hamuli wa Wizara ya Maji na wataalamu wengine kutoka DAWASA na kampuni za Uhandisi.
Mabomba yaliathirika baada ya mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa wiki eneo la Jangwani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Bashir Mrindoko (wa pili kulia) akiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Jackson Midala (wa kwanza kushoto) walipotembelea eneo la Jangwani kkuangaliaa mabomba yalioathirika na mvua.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Bashir Mrindoko akipata maelekezo kutoka kwa Mhandisi ya namna ya kukarabati mabomba yaliyokatika eneo la Jangwani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Bashir Mrindoko akiwa katika masikitiko makubwa mara baada ya kujionea athari kubwa ya kukatika kwa mabomba iliyotokea Jangwani baada ya mvua kubwa zinazonyesha jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad