Wadau wanaohudhuria Mkutano Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF wakipata huduma ya kupimna afya bure kwenye banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Wadau wakiwa kwenye harakati za kujua afya zao na kupata ushauri.
Wadau wa mkutano huo wakiwa kwenye foleni ya kupima afya bure kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa PSPF uliozinduliwa jana na Rais Mstaafu All Hassan Mwinyi.
Wakipata vipimo vya sukari na shinikizo la damu.
Maofisa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wataalam kutoka Hospitali ya Amana wakitoa huduma kwa wadau hao.
Maofisa Masoko na Elimu kwa Umma, Hawa Duguza na Grace Michael wakitoa maelezo kwa wanachama wa Mfuko huo.
Wadau hao wakiendelea na huduma za kujua afya zao na kupata ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Na Mwandishi Wetu
WADAU wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuendesha zoezi la upimaji afya bure katika Mkutano huo.
Mkutano huo uliojumuisha wadau mbalimbali na baadhi yao wakiwa ni wanachama wa NHIF, wamesema kitendo hicho ni kizuri kwa kuwa kinalenga kuwaelimisha wananchi namna ya kuishi katika mtindo bora wa maisha ya kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ambayo kwa sasa ni tishio kubwa.
Wakipata huduma bandani hapo, wameuomba Mfuko kueneza fursa hiyo katika maeneo mbalimbali ili wananchi wajue afya zao hasa katika maeneo ya vijijini ambako fursa kama hizo zimekuwa ni ngumu kufika.
Hata hivyo akizungumza bandani hapo Meneja wa NHIF Kanda ya Ilala, Christopher Mapunda alisema kuwa Mfuko kwa sasa una mpango maalum wa kuelimisha wananchi na wanachama wake namna ya kujikinga na maradhi hayo lakini pia kuendesha upimaji wa afya bure katika maeneo mbalimbali yakiwemo na kijijini.
Alisema kuwa Mfuko umefikia hatua ya kuendesha mpango huo kutokana na ukweli kwamba magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka kila kukicha na gharama zake za matibabu ni kubwa ambazo kwa wananchi wa kawaida ni ngumu kuzimudu.
“Elimu hii na huduma ya upimaji tunajitahidi kufika katika maeneo mengi kupitia ofisi zetu za mikoa hivyo ni vyema wananchi wakatambua umuhimu wa kupima afya zao wakati fursa kama hii inapotokea katika maeneo yao,” alisema Mapunda.
Upimaji unaofanywa na NHIF ni sukari, shinikizo la damu, uzito na urefu ambapo wanaobainika kuwa na matatizo wanapewa ushauri wa namna ya kufanya ili kupunguza tatizo ama kuepukana nalo.
Katika Mkutano huo wa PSPF zaidi ya wadau 200 wamepata huduma ya kujua afya zao lakini pia elimu zaidi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hususan uboreshaji wa mafao unaofanywa na Mfuko ili kukidhi mahitaji ya wanachama wake.
No comments:
Post a Comment