HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 27, 2014

WAZIRI CHIKAWE APOKEA MADARAKA RASMI KUTOKA KWA DKT. NCHIMBI

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe, Dkt Emmanuel Nchimbi akizungumza jana na wakuu wa idara za wizara hiyo baada ya kukabidhi rasmi ofisi kwa Waziri Mathias Chikawe aliyeteuliwa na Rais hivi karibuni kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi. 

Na, Hassan Mndeme  na Tumaini Julius – Jeshi la Polisi

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe, Emmanuel Nchimbi ameahidi kushirikiana na Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi katika kuihimiza Serikali kuongeza bajeti ya wizara hiyo kwani anafahamu umuhimu wa wizara hiyo na changamoto zinazoikabili.

Alisema hayo kwenye kikao kilichofanyika  jana Makao Makuu ya Jeshi la  Polisi baada ya  makabidhiano na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe  baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa waziri wa wizara hiyo.

Aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ni wizara muhimu  katika mustakabali wa amani ya nchi hivyo ikiwa na bajeti ya kutosha  itaweza kuwajengea watendaji  mazingira mazuri  ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi yao na kuongeza  ufanisi, uaminifu  na uadilifu katika utendaji wao wa kila siku.

Aidha, alisisitiza kuwa misingi na wajibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kutoa haki kwa raia, wizara ikikalia haki nchi haitakalika, hivyo raia wanapaswa kupewa haki zao kwa wakati unaostahili kwani ni njia mojawapo ya kujenga ushirikiano na jamii na kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Pia, Mhe Nchimbi amewataka wananchi kufuata sheria katika kutafuta haki zao badala ya kujichukulia sheria mkononi na kuwa serikali itawachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kushiriki katika vitendo vya kihalifu.

Awali akimkaribisha aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe, Mathias Chikawe alihaidi kutoa ushirikiano kwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa haki kwa raia kwa wakati unaostahili bila upendeleo ili kutoa uduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Amme Silima amewataka watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanya shughuli zao kwa kufuata maadili, sheria na kanuni za kazi zao ili wananchi waweze kupata huduma wanazostahili.

Silima  aliongeza  kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili Wizara ya mambo ya ndani ni ufinyu wa bajeti, tabia za wananchi kujichulia sheria mkononi, matukio ya kufunga Barabara, mauaji ya kulipiza visasi au kuadhibu watu wanaotuhumiwa kuwa wahalifu na kusema vitendo kama hivyo havipaswi kuvumiliwa kwa vile vinaweza kusababisha machafuko makubwa hivyo wizara inapaswa kuandaa mikakati ya haraka ya kukabiliana na hali hiyo kabla haijasababisha madhara makubwa katika jamii.

  Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Pereira Amme Silima, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mwamini Juma Malemi, makamanda wa Vyombo vya dola vilivyopo Wizara ya Mambo ya Ndani na wakuu wa idara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad