Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Pindi Chana akimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Hamis Mdee muda mfupi baada ya kutembelea banda la Mfuko huo.
Ofisa Matekelezo Desiderius Buhiye akitoa maelezo ya shughuli zinazofanywa katika banda la NHIF kwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru wakiendelea kupata huduma ya kupima afya zao.
Upimaji ukiendelea
Ofisa Matekelezo wa NHIF akitoa elimu kwa Maofisa wa Maendeleo ya Jamii waliofika bandani hapo kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali.
SERIKALI imesema itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hususan za kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko huo pamoja na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili wanufaike na huduma za matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Pindi Chana wakati alipotembelea banda la NHIF katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru ambayo yamekwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa Maofisa Maendeleo ya Jamii nchini.
“Juhudi mnazofanya ni kubwa na kwa upande wetu tuko tayari kabisa kuwaunga mkono na kwa kuwatumia hawa Maofisa Mendeleo ya Jamii naamini wananchi wataelewa na kujiunga na huduma hizi ili wawe na uhakika wa kupata matibabu,” alisema Dk. Chana.
Katika maadhimisho hayo, NHIF inatoa huduma za upimaji wa afya bure, kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza pamoja na elimu inayolenga faida za kuwa katika utaratibu wa kupata matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mfuko wa Afya ya Jamii na Tiba kwa Kadi.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee, alitumia mwanya huo kuwaomba Maofisa Maendeleo ya Jamii kuhamasisha wananchi kujiunga na Mifuko hiyo kwa kuwa ndio njia pekee ya kumkomboa mwananchi na kumfanya awe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.
“Mtaji wa mwananchi yoyote ni afya yake mwenyewe, huwezi ukafanya shughuli zozote za kimaendeleo bila kuwa na afya njema…gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa hivyo njia ya uhakika na rahisi ni kujiunga na mifuko hii na kwa upande wetu kama NHIF tunaendelea na uboreshaji wa huduma zetu ili kuondokana na changamoto chache zilizopo,” alisema Mdee.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Maofisa Maendeleo waliofika katika banda la NHIF, waliupongeza Mfuko kwa kuweka huduma hiyo ambayo imewasaidia kujua afya zao lakini pia kupata majibu ya maswali waliyokuwa nayo kuhusiana na huduma za NHIF.
Akizungumza bandani hapo Bw. Elias Lotaa alisema ni wakati sasa kwa NHIF kuhakikisha inakwenda zaidi katika maeneo ya vijijini kuhamasisha wananchi kujiunga na Mifuko hii kwa kuwa inayo manufaa makubwa.
“Mimi ni shuhuda mzuri wa huduma nilizopata kutoka NHIF, gharama nilizolipiwa kwa ajili ya matibabu ya mke wangu ni kubwa ambayo kwa hali ya kawaida ingeniwia ngumu sana hivyo nawahamasisha sana wananchi kujiunga na Mfuko huu lakini na nyie NHIF ongezeni bidii ya kufikia makundi mengi wakiwemo wakulima na wafugaji,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa elimu kwa umma, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Christopher Mapunda alisema kuwa NHIF inaendelea na mikakati mbalimbali ya elimu ikiwemo ya Elimu ya kata kwa kata ambayo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa suala la utoaji wa elimu kwa NHIF ni endelevu hivyo akawaomba wananchi kutumia fursa zilizopo kujiunga na huduma za Mifuko hii. “Kwa sasa tumesogeza sana huduma kwa wananchi kwa kufungua ofisi katika mikoa 25 hivyo tunaamini changamoto nyingi za wanachama wetu zinatatuliwa kwa uharaka,” alisema Bw. Mapunda.
No comments:
Post a Comment