HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 22, 2013

MADAKTARI BINGWA WA UPASUAJI MUHIMBILI WAPIGWA MSASA KUHUSU MAGONJWA YA MATITI

Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamepigwa msasa kuhusu tiba ya magonjwa mbalimbali ya matiti ili kuongeza ujuzi na weledi katika magonjwa hayo.

Akifungua semina ya siku nne inayoendelea Hospitalini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Marina Njelekela alisema kuna magonjwa mengi yanayoshambulia matiti yakiwemo vivimbe, maambukizi, saratani n.k.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Njelekela akifungua semina.

Alisema saratani ya matiti inaongoza kwa kuwa na waathirika wengi zaidi ukilinganisha na saratani nyingine na inaathiri wanawake na wanaume pia.  

Dkt. Njelekela alisema katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 2012 hadi Juni 2013, wagonjwa 856 walifanyiwa upasuaji katika vitengo viwili vya ndani ya idara ya upasuaji na kati yao 162 sawa na asilimia 14.9 walikuwa na saratani ya matiti.

Alisema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ugonjwa wa saratani ya matiti ni mojawapo ya ugonjwa unaongooza kati ya magonjwa 10 katika Idara ya Upasuaji kwa wanawake hivyo juhudi zozote zinazoelekezwa kupambana na ugonjwa wa saratani ya matiti zinahitaji kupongezwa.

Dkt. Njelekela alisema kupata ujuzi kazini katika kuboresha weledi wa wataalam ni wa muhimu sana kwani kuna mabadiliko mengi yanayoendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Semina hii Dkt. Julieth Magandi.

Mwezeshaji wa semina hii Prof. Zervoudis Stephane ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama na pia amebobea kwenye magonjwa ya matiti alisema elimu ya magonjwa ya saratani ya matiti ni ya muhimu sana kwani kila siku idadi ya wanaougua inaongezeka hivyo kupitia semina hii itawezesha kupunguza tatizo kwani watu wataelewa umuhimu wa kupima na kuchukua hatua mapema.
Mwezeshaji wa semina hii Prof. Zervoudis Stephane ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama na pia amebobea kwenye magonjwa ya matiti akitoa mada kwa washiriki wa semina hiyo.

Semina hii inawajumuisha madaktari walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo, Madaktari kutoka Hospitali za Amana, Temeke, Mwananyamala na Hospitali binafsi zilizoko Jijini Dar Es Salaam pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Baadhi ya Washiriki wa semina wakimsikiliza mtoa mada.
Picha ya pamoja ya washiriki wa semina hiyo: Wanne kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Mairna Njelekela ambapo kulia kwake ni Mwezeshaji wa Semina Prof. Zervoudis Stephane.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad