Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Uganga wilayani Makete akizungumza na mwandishi wetu kuhusu tatizo la upungufu wa waaalimu shuleni hapo.
Mwalimu Yuda Kiluswe ambaye anafundisha darasa la awali hadi la pili akiwa darasani akifundisha.
Edwin Moshi wa Michuzi Media, Makete.
Tatizo
la upungufu wa waalimu katika shule mbalimbali wilayani Makete mkoani
Njombe limezidi kushika kasi baada ya shule ya msingi Uganga kata ya
Luwumbu wilayani hapo kuwa na waalimu wanne tu na wote wakiume licha ya
shule hiyo kuwa na wanafunzi wa kike na wakiume.
Tukio
hilo la aina yake limedhihirika baada ya mwandishi wa mtandao huu
kufunga safari na kwenda shuleni hapo na kuwakuta waalimu hao
wakijitahidi kufundisha wanafunzi ambapo jumla ya wanafunzi wote wapo
112.
Mwandishi
wetu ameshuhudia mwalimu Yuda Kiluswe ambaye ni mwalimu wa darasa la
awali, la kwanza na la pili, akiwafundisha wanafunzi jambo
lililomshangaza mwandishi na kwenda kumhoji kulikoni yeye kama mwalimu
mwanaume anawafundisha wanafunzi wa darasa la awali hadi la pili ili
hali imezoeleka wanafunzi wa madarasa hayo hufundishwa na waalimu wa
kike.
Mwalimu
Kiluswe amesema analazimika kufundisha madarasa hayo kwa kuwa hakuna
mwalimu wa kike shuleni hapo hivyo kulazimu waalimu hao wane waliopo
shuleni hapo kufanya kazi zote za kufundisha pamoja na misaada yote
wanayohitaji wanafunzi wawapo shuleni hapo.
“Ni
kweli imezoeleka wanafunzi hawa wadogo wanafundishwa na waalimu wa
kike, lakini kwa kuwa hawapo je tufanye nini, hapa hakuna cha kufanya
zaidi ya mimi kuingia darasani na kuwafundisha na wameshazoea na hata
mimi pia nimeshazoea” alisema mwalimu Kiluswe.
Akizungumzia
suala hilo mwalimu mkuu wa shule hiyo Eliuda Daniel Msigwa amesema ni
kweli kuwa shule hiyo ina waalimu wane wote wa kiume wanaohudumia
wanafunzi 112 wanaosoma shuleni hapo.
Amesema
ni kweli wameshatoa taarifa wilayani kuomba kupatiwa mwalimu wa kike
hata mmoja lakini bado kilio hicho hakijasikika hivyo kuiomba
halmashauri ya makete kuona namna ya kufanya kuwapa waalimu wa kike hata
kwa kuhamisha kutoka shule nyingine na kuwapeleka shuleni hapo.
“Ni
kweli tunajua kuwa waalimu hawatoshi lakini mimi ningeshauri, hapa tuna
waalimu wanne wakihamisha hata mmoja wa kiume na kumleta mwalimu wa
kike badala yake, hii itasaidia wakati tunasubiri serikali kupangia
waalimu wengine wapya shuleni hapa” alisema mwalimu mkuu.
Amesema
mbali na kuwepo waalimu wanne bado hawatoshi na kusema wakiongezeka
angalaua watatu kutawarahisishia kupungua kwa kazi nyingi kwani
wanafanya kazi kupita kiasi kutokana na uchache wao.

No comments:
Post a Comment