Na Mwandishi Maalum
Wakati watanzania wakiwa bado hawajawasahau mashujaa wao Saba waliopoteza maisha wakati wakitekeleza jukumu la ulinzi wa Amani ya kimataifa katika jimbo la Darfur, nchini Sudan, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, limetoa wito kwa walinzi wa Amani kudhibiti mashambulizi yanayoelekezwa dhidi yao.
Wito huo wa Baraza Kuu la Usalama umo ndani ya Aya zipatazo 30 za Azimio namba 2113 la mwaka 2013 ambalo limeongeza muda wa Mamlaka ( Mandate) ya Misheni ya Mseto ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika inayolinda Amani katika Jimbo la Darfur maarufu kama UNAMID.
Katika kikao chake kilichofanyika siku ya jumanne, wajumbe 15 wanaounda Baraza Kuu la Usalama walipitisha kwa kauli moja Azimio hilo linaloongeza mamlaka ya UNAMID kwa miezi 13 hadi Agosti 31, 2014.
Miongoni mwa Aya hizo 30 zipo aya zinazoelezea kwamba ingawa kumekuwa na hali ya utulivu tangu Misheni ya UNAMID ilipopelekwa Darfur lakini pia limeeleza kusikitishwa kwake na uwepo wa matukio ambayo yanaelekea kudhoofisha hali ya amani na usalama na vile vile kuvuruga shughuli za ulinzi wa amani na upelekaji wa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wanaokubwa na machafuko hayo.
Baraza Kuu kupitia Azimio hilo pamoja na mambo mengine limelaani vikali matukio ya kushambuliwa kwa walinda Amani wa UNAMID, likiwamo tukio la hivi karibuni la Julai 13, ambapo walinda amani saba walipoteza maisha na wengine 14 akiwamo polisi kujeruhiwa katika shambulio la kushitukiza.
Azimio hilo pia limesititiza mamlaka ya UNAMID ambayo yapo ndani ya Sura ya VII ya Katiba ya Umoja wa Mataifa, na kutoa wito kwa walinzi hao wa amani kuzuia vitisho vyovyote dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwalinda wananchi walio hatarini bila kuathiri wajibuwa wa serikali wa kuwalinda wananchi wake.
Aidha Baraza Kuu limesisitiza kupitia Azimio hilo haja na umuhimu kwa walinzi wa Amani wa siyo tu kuwa tayari kukabili vitisho dhidi yao, bali limevitaka vyombo vinavyohusika kuhakikisha kuwa walinzi hao wanapewa zana na vifaa vitakavyowawezesha kutekeleza mamlaka waliyopewa.
Vile vile kupitia Azimio hilo Baraza limerejea tena wito wake wa kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tukio la Julai 13, na kwamba ni matumaini yake kuwa serikali ya Sudan itashiri kikamilifu kama ambavyo imekwisha kuahidi. Na aidha Baraza limeyataka makundi mengine kutoa ushirikiano huku likisisitiza kwamba hujuma dhidi ya walinzi wa amani ni jambo ambalo halikubaliki.
Katika muktadha huo, na kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu la usalama limezitaka pande husika na hasa makundi yenye silaha na ambayo hayajatia saini Nyaraka za Doha kuhusu amani ya Darfur , kuacha mara moja vitendo vyovyote vinavyolenga kuvuruga Amani na kukomesha unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji holela.
Vile vile na makundi hayo yametakiwa kushiriki bila ya kuchelewa na bila masharti katika mazungumzo ya kuteta Amani.
Aidha Azimio hilo linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika kuendelea kupitia utekelezaji wa Mamlaka ya UNAMID ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa Baraza hilo kila baada ya siku tisini.
Kupitia Azimio hilo Baraza Kuu limezishukuru nchi zote ambazo zimetoa wanajeshi wake na polisi kushiriki katika operesheni ya kulinda amani kupitia UNAMID na limeyaomba mataifa mengine kuendelea kuchangia kwa hali na mali ili hatimaye UNAMID iweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu na kufanya Darfur kuwa mahali salama.
Wakati huo huo akizungumza baada ya Azimio hilo kupitishwa, Muwakilishi wa Jamhuri ya Sudan katika Umoja wa Mataifa, Bw. Daffa-Alla-Elhag Ali Osman, amelihakikishia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwamba serikali yake itashiriki kikamilifu katika kuwasaka wale wote waliohusika na tukio la Julai 13.


No comments:
Post a Comment