Na Thehabari.com, Kishapu
WASUKUMA ni moja
ya makabila nchini Tanzania ambayo awali yalishikilia desturi ya
familia kuwa na idadi kubwa ya watoto. Familia moja yaani baba na mama
waliendelea kuzaa kadri walivyo jaaliwa kupata watoto bila kujali ukubwa
wa familia. Mume pia hakuwa na kizuizi katika familia cha kuongeza mke
mwingine endapo atakuwa na ardhi (mashamba) na mifugo (hasa ng'ombe) ya
kutosha kuweza kuihudumia familia aliyonayo.
Wapo walioamini kwamba kuwa na ukubwa wa familia ni
kuongeza nguvu kazi katika uzalishaji kwa kutumia ukubwa wa familia.
Hata hivyo pia wapo walioamini uzazi ni mpangilio wa Mungu hivyo
haupaswi kupangiliwa na wazazi bali mola mwenyewe. Hivyo basi familia za
imani hii ziliendelea kuza hadi pale uwezo wa kupata watoto ulipopotea
wenyewe au vizuizi vingine.
Hata hivyo sasa hivi mambo yamebadilika kiuchumi,
hali ni ngumu hivyo familia nyingi zinapangia idadi ya watoto.
Waliojisahau na kuendelea kuzaa idadi kubwa ya watoto pasipo na uwezo
kuwamudu wanajuta na kutamani wangelipata uelewa wa elimu hiyo awali.
Bi. Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso ni
miongoni mwa familia zinazojutia uamuzi wa kuwa na idadi kubwa ya
watoto. Anasema familia yao ilikuwa na jumla ya watoto 10, lakini bahati
mbaya wawili walifariki dunia hivyo kubakia na watoto nane ambao ni
mzigo mkubwa hivi sasa.
"...Hatukuwa na elimu ya kupangilia watoto tulizaa
mfululizo kadri ya tulivyo jaaliwa, lakini watoto hawa sasa ni mzigo
kwetu, tunajuta. Tumeshindwa kuwasomesha na wamekosa muelekeo...na hata
upatikanaji wa chakula cha familia nzima ni tatizo...hasa ukichangia na
hivi karibuni ukame uliibuka eneo hili mambo yamezidi kuwa mabaya,"
anasema Bi. Moshwa.
Paschal Kulwa Manyinzi (42) ni mume wa Bi. Rejina
Moshwa, anasema licha ya kuwa na mifugo kidogo yeye ni mkulima wa mazao
mchanganyiko yaani Pamba, mtama, karanga na viazi. Anakiri watoto wake
mwenyewe kuwa mzigo mkubwa kimalezi kwa sasa. "Wakati tunaanza kuzaa
nilifuata mila na desturi za zamani, unajua zamani suala la kuzaa
halikuwa la kupangilia, mtu ulikuwa unazaa tuu...suala la kupangilia
limeanza juzi.
"Zamani (enzi za wazazi wetu) idadi kubwa ya watoto
katika familia ilikuwa ni nguvu kazi...lilikuwa likizaidia katika
kilimo...kama mtu ulikuwa hauna familia kubwa ulitapata shida kwenye
kilimo. Lakini dunia ya sasa huwezi kuzaa kama mimi ni mzigo," anasema
Manyinzi.
Hata hivyo licha ya ukubwa wa familia hii haina
ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwani heka tano ambazo inadai
ilipewa kwa urithi toka kwa wazazi wa Manyinzi imetwaliwa na Serikali
kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kubaki heka moja. Familia hii
inalazimika kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo kila msimu wa kilimo.
Modesta Machia (43) ni Mkazi wa Kijiji cha Kishapu,
Kata ya Kishapu Wilaya ya Kishapu. Anasema yeye na mumewe wana jumla ya
watoto nane walio hai kati ya 10 ambao walibahatika kuwazaa. Anasema
watoto wawili walitangulia mbele za haki. Anasema watoto walionao kwa
sasa ni mzigo katika malezi.
"...Mwanzoni tulikuwa tunazaa haraka haraka kwa kuwa
hatukuwa na uelewa juu ya uzazi wa mpango...lakini laiti ningejua
nisingelikubali kupata idadi kubwa ya watoto kama ilivyo sasa...lakini
nimepata uelewa nikiwa nimechelewa na nimefunga kizazi kabisa," anasema
Bi. Machia. Anasema mume wake kwa sasa ni muhudumu wa usafi katika
zahanati ya kijiji chao.
Mwanamama huyu anashauri familia nyingine kuzaa kwa
mpangilio na kuzingatia kipato cha familia ili kupunguza umaskini wa
kiuchumi katika familia. Anasema mwanamke kuzaa mfululizo hushindwa
kuchangia shughuli za kujiongezea kipato katika familia na hata kuchoka
mapema kwenye shughuli za uzalishaji mali.
Hata hivyo changamoto nyingine kwa uzazi wa idadi
kubwa ya watoto ipo kwa akinamama pekee, kwani inapotokea mke na mume
wakatofautiana na kufikia kuachana, idadi kubwa ya kinababa humuachia
mke watoto waliozaa na yeye kwenda kuoa sehemu nyingine.
Bi. Paskazia John mama mwenye watoto nane amekubwa
na hali kama hiyo, kwani baada ya kuzaa na mumewe watoto nane
walikorofishana na kutengana hivyo mwanaume kumuachia watoto wote nane
ambao kwake ni mzigo mara dufu. Anasema unapoolewa katika familia ya
kisukuma hasa maeneo ya vijijini kuzaa idadi kubwa ya watoto ni kitu cha
kawaida. Anaongeza kuwa na endapo utaonekana mvivu wa kuzaa mwanaume
anaweza kukuongezea mke mwenzako ili akusaidie.
Anabainisha kuwa baadhi ya wanaume wa kisukuma
wanaamini kwamba kuwa na idadi kubwa ya watoto ni sawa na kuwa na uwezo
kiuzalishaji, yaani watoto watatumika kama nguvu kazi shambani. Lakini
kwa kuwa kaya nyingi za maeneo ya wasukuma mama (mke) pamoja na watoto
huwa ndiyo watendakazi wakubwa mashambani huku baba akibaki kuwa
msimamizi na kiongozi wa familia wanawake ndiyo wenyemzigo mkubwa katika
familia nyingi za kuangaika na watoto.
Hata hivyo si familia zote zenye mzigo mkubwa wa
watoto wanashindwa kuzimudu. Ally Sosoma (60) ni mkulima na mkazi wa
Kijiji cha Isoso, katika familia yake ana jumla ya watoto 20 ambao
wamepatikana ndani ya wake watatu. Anasema familia yake imeanza kuwa
mzigo mkubwa kwake baada ya kuanza ukame mfululizo yaani mwaka 2011 hadi
sasa. Anaongeza kuwa hapo nyuma haikuwa mzigo kwa kuwa alikuwa
anajituma na ardhi ya kutosha hivyo alizalisha chakula na ziada ya
kutosha jambo ambalo haikuwa tabu kuendesha familia yake.
Anasema mila na desturi ya kuwa na idadi kubwa ya
watoto ameirithi kutoka kwa baba yake ambaye alikuwa na wake watatu.
"...Pamoja kwamba baba alikuwa na wake watatu lakini baba yangu mkubwa
alikuwa na wake saba hivyo alikuwa na watoto wengi sana, hivi ndio
chanzo cha kuwa na idadi kubwa ya watoto...mimi nilipenda na ndiyo maana
nimezaa wengi. Lakini si kweli kwamba watu wanasema ukioa mwanamke wa
kisukuma na kutozwa ng'ombe nyingi lazima akuzalie watoto wengi,"
anasema Sosoma.
Kwa upande wake, Yamesa Sheka mkulima mkazi wa
Kishapu; anasema mila na desturi za kuwa na idadi kubwa ya watoto kwa
sasa zimepitwa na wakati kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Idadi kubwa ya watoto inachangia umaskini katika familia nyingi kwa kile
wazazi kushindwa kuwahudumia watoto. Kijana huyu anawatoto saba kwa
sasa lakini anajuta kuwapata kwani ni mzigo kuwalea. "...Ningelipata
elimu ya uzazi mapema ningelikomea watoto wanne tu, lakini haikuwa
hivyo," anasema Sheka.
Maxmilian Lugembe ni Ofisa Mtendaji Kata ya Kishapu,
akizungumzia utaratibu wa familia kuzaa idadi kubwa ya watoto anasema
inachangiwa na mfumo dume ambao wameuendekeza familia nyingi za
kisukuma. Anasema katika mfumo huo baba ndiye mwenye maamuzi ya kuongeza
watoto bila kushauriana na mwenza wake.
"...Maeneo haya familia kuwa na watoto 10 au 8 ni
kitu cha kawaida. Elimu inatolewa ya uzazi wa mpango ambayo anaipata
mama pekee lakini kutokana na mfumo dume mama hana uamuzi katika familia
hivyo unakuta aisaidii...kwanza wanaume hawataki wake zao kujiusisha na
uzazi wa mpango (kutumia dawa kupanga uzazi) na wengine wakifanya kwa
siri na kugundulika unakuwa ugomvi mkubwa," anasema Lugembe.
"Inafikia wakati hata wanawake wanaoonekana kupanga
uzazi katika ndoa zao wanaaminika kuwa ni wahunu, yaani wanataka
kupumzika kuzaa ili wapate nafasi ya kufanya maovu (uhuni) nje ya ndoa.
Wapo wanaoamini kuwa ishara ya kumpenda mwanaume ni kumzalia
watoto...unazaa uwezavyo hadi uchoke," anasema.

No comments:
Post a Comment