Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania (ILO) Bw. Alexio Musindo amesema kupitia msaada kutoka Serikali ya Sweden wa kifedha ILO iliweza kuwahusisha wasichana na wavulana katika makundi mbalimbali wenye vipato vidogo kupata uelewa wa Afya ya Uzazi kupitia Makongamano, Semina na Mafunzo mbalimbali yaliyoendeshwa na shirika hilo la kazi Duniani.
Ameongeza kuwa “tuliwasaidia kuwaunganisha na vikundi vya kuweka na kukopa ili waweze kupata mitaji midogo midogo ya kufungua biashara ndogo ndogo katika harakati za kuwafanya wajitegemee na kuepekana na vishawishi vya Ngono isiyokuwa Salama.
Bw. Musindo amesisitiza Umuhimu wa TACAIDS kuandaa makongamano kama haya ili kuwawezesha wasichana na wavulana wadogo kupata ufahamu uelewa na mafunzo ya uzazi wa Afya na jinsi ya kuelewa mabadiliko yao ya kimaumbile.
“Ni matumaini yangu mwingiliano huu wa Utamaduni wa kupambana na Ukimwi, Kinga na Uwezeshwaji wa Kiuchumi umefanyika vizuri, hasa katika kuyalenga makundi yaliyo katika mazingira magumu itasaidia kuongeza kasi ya kupunguza maambukizi mapya kama ilivyoripotiwa na ripoti ya UNAIDS mwaka 2012 Duniani kwamba maambukizi mapya yamepungua kwa Asilimia 20”. Amesema.
Mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Kijakazi Mtengwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo amesema mikakati ya kuwawezesha Wanawake Kiuchumi inaweza kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa Wanawake, Wasichana na Wavulana wadogo.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa leo kwenye Kongamano hilo.




No comments:
Post a Comment