HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 9, 2013

Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia yalitaka Jeshi kuwa Mfano wa kuendeleza Teknolojia nchini

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Profesa Patrick Makungu (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa msafara wa wanafunzi toka Chuo cha Uongozi wa Juu wa Kijeshi cha Ghana, Brigedia Jenerali A. Annan jana jijini Dar es Salaam.  Wanafunzi hao walitembelea wizara hiyo kama moja ya ziara yao ya mafunzo hapa nchini.
Kiongozi wa msafara wa wanafunzi toka Chuo cha Uongozi wa Juu wa Kijeshi cha Ghana, Brigedia Jenerali A. Annan (Kulia) akiongea wakati ujumbe wake ulipotembelea Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano jana jijini Dar es Salaam.  Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Patrick Makungu na Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia wizarani hapo Prof. Evelyne Mbede.

 Jeshi la Wananchi wa Tanzania limetakiwa kuendelea kuwa katika mstari wa mbele katika kuendeleza ubunifu wa kisayansi ili kuharakisha juhudi za kujiletea maendeleo lenyewe na taifa kwa ujumla.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Profesa Patrick Makungu ameyasema hayo alipotembelewa na wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Juu wa Kijeshi cha Ghana ambao wapo nchini katika ziara ya mafunzo.

 Profesa Makungu amelitaka jeshi kufanya kazi nyingine zaidi ya kazi zao za kijeshi ili kuweza kuisaidia nchi na jamii kujiletea maendeleo. “Jeshi linapaswa kuchukua nafasi ya kwanza kabisa katika juhudi za kuunganisha bara la Afrika kupitia sayansi na techinolojia,” alisema. 

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia katika Wizara hiyo, Profesa Evelyne Mbede amewakumbusha wanajeshi hao kuwa maendeleo yaliyopatikana leo katika sekta ya teknolojia ni matunda ya tafiti za awali zilizokuwa zikifanyika jeshini. 

Amelitaka jeshi la wananchi wa Tanzania kuendeleza moyo wa kukuza teknolojia kupitia mashirika yake ya Mzinga na Nyumbu ambayo yamekuwa kielelezo cha wazi kabisa ya jinsi jeshi linavyojihusisha na maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini. 

Akiongea kwa niaba ya ujumbe wa wanafunzi hao,mwambata wa kijeshi wa nchi ya Ghana katika Ubalozi wa Ethiopia, Brigedia Generali A.Annan, amesema kuwa Afrika kwa sasa inahitaji kuwa moja kwa kuweza kuunganisha rasilimali na nguvu pamoja ili kuwa na sauti. 

Ameongeza kuwa ndoto yake ya muda mrefu ni kuona Afrika inakuwa na sarafu moja huku vikwazo vya kimipaka navyo vikiondolewa ili kuwezesha watu kuvuka mipaka toka sehemu moja kwenda nyingine. Awali akiwasilisha mada juu ya jinsi ya kuboresha mahusiano na maendeleo ya afrika kupitia sayansi na techinolojia.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti katika wizara hiyo, Bwana Raphael Chibunda amesema Afrika ina nafasi nzuri ya kutatua matatizo yake pamoja kupitia sayansi na teknolojia. Amesema nchi kama Rwanda imepiga hatua kubwa kutokana na kuwepo sera bora za maendeleo pamoja na teknolojia. 

 Amesema sayansi na teknolojia vina nafasi kubwa ya kuweza kuboresha maisha ya watu wa kawaida na kuyafanya yawe bora. Ujumbe huo ulikabidhiwa zawadi na Profesa Makungu na baadae ujumbe huo uliweza pia kutoa zawadi kwa Wizara hiyo. 

Ni utaraibu wa kijeshi kwa wanafunzi wake katika kozi za ngazi ya uongozi wa juu kutembelea nchi mbalimbali ambapo wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanapata nafasi ya kutembelea mataifa mengine kwa lengo la kujifunza. Msafara huo ulijumuisha wanafunzi wa mataifa mbalimbali wanaoshiriki mafunzo katika chuo hicho. Mataifa hayo ni Ghana,Nigeria, Rwanda,Tanzania, Mali na Afrika ya kusini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad