Tarehe
kama hii, miaka mitano uliyopita,mama mpendwa Adelina Mapango, uliagana
nasi. Nikisema 'uliagana nasi' inaweza kutafsiriwa kana kwamba ulipata
nafasi ya kutuaga.Nilikuja huko nyumbani kukuuguza Februari 2008, lakini
tangu nilipokuona pale Muhimbili hadi tarehe 29 Mei 2008 hukuwahi japo
kuniambia neno moja la mwisho.Nakumbuka ulivyokuwa ukiniangalia kwa
upendo wako mkubwa,nakumbuka pia tabasamu lako licha ya maumivu makubwa
uliyokuwa nayo.Lakini kila nilipojaribu angalau kusikia neno lako moja
tu,haikuwezekana hadi siku unafariki.
Mama
mpendwa, kabla ya kifo chako sikuwahi kuelewa maana ya kufiwa na mzazi
au mtu wa karibu.Sasa sio tu naelewa bali kila siku ya Mungu tangu siku
ulipotutoka imekuwa kama ndoto mbaya ambayo natamani iishe ili hali
irejee kuwa kama zamani.Kwa bahati mbaya, ndoto hiyo mbaya ni ukweli
(hali halisi), na hadi sasa matarajio kuwa kuna siku nitaamka na kukuona
au kukusikia ukiwa hai yanazidi kufifia.Kwa kifupi,mama mpendwa,hadi
leo bado napata shida kuamini na kukubali kuwa haupo nasi.
Nyakati
mbili ngumu zaidi kwangu ni wakati ninapofanya sala kabla ya kulala
ambapo wakati wa uhai wako nilikuwa nikisali "Ee Bwana uijalie familia
yangu yani Baba na Mama..." lakini sasa inabidi nimtaje Baba pekee.Pia
wakati wa uhai wako,nilijenga utaratibu
kwamba nikipiga simu naanza kuongea na Baba kisha anapitisha simu kwako
tunaanza kutia stori mbalimbali.Sasa,mama, nikimaliza kuongea na
Baba huwa najikuta nasahau kuwa haupo hapo nyumbani,na kumwambia Baba
akupe simu...then nakumbuka haupo.Naishia kutoa machozi.
Nikiwa
mbinafsi,nitaangalia tu jinsi ninavyopata shida kukabiliana na ukweli
kuwa hauko nasi.Lakini kuna rafiki yako kipenzi Baba Mzee Chahali ambaye
yeye amekuwa mtu tofauti kabisa tangu ulipoondoka.Kama
unavyokumbuka,baba ni mtu mkimya,mwenye marafiki wachache, na rafiki
yake mkuu ulikuwa wewe.Sasa tangu uondoke,baba amekuwa mnyonge kupita
kiasi.Kibaya zaid, ameendelea kudai labda yeye ndio angestahili
kutangulia mbele ya haki kwa vile alikuwa amekuzidi kiumri.Kwa hakika,
baba ameendelea
kuwa katika wakati mgumu sana licha ya sapoti kubwa tunayompatia.
Lakini
pia kuna rafiki zako wapenda Kulwa na Doto (Peter na Paul). Pengine kwa
vile wao ni last borns, walikuwa wakikuchukulia zaidi ya mzazi, ulikuwa
kama bibi yao, shangazi yao, na kikubwa zaidi, rafiki yao.Kila
ninapoongea na wadogo zangu hawa najiskia kutokwa na machozi.Kimsingi,
sidhani kama waliwahi kuwaza kuwa na maisha bila ya uwepo wako mama.
Familia
yote kwa ujumla inakukumbuka sana mama.Nina mkanda wa video
niliowarekodi wewe na baba mlipokuwa mnaadhimisha miaka 50 ya
ndoa yenu mwaka 2005,lakini kila nikijaribu kuuangalia najikuta
nabubujikwa na machozi.Katika mkanda huo uliongea mambo mengi ya msingi
kuhusu maisha.Kuna nyakati nataka kuuangalia ili nirejee wosia wako
lakini nashindwa kwa sababu ya uchungu.
Mama
nilikupenda sana,ninakupenda sana,na nitaendelea kukupenda
milele.Kwangu, japo hupo nasi kimwili,lakini unaendelea kuishi nasi
kiroho.Nitazidi kukukumbuka kwa sala kila siku,na ninaamini huko uliko
unapata faraja kila ninapotenda mambo kwa kuzingatia mafundisho yako.
WE MISS YOU SO MUCH MAMA MPENDWA
PUMZIKO LA MILELE AKUPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE UPUMZIKE KWA AMANI AMINA
No comments:
Post a Comment