Na Edwin Moshi,Makete.
Serikali wilayani Makete imesema haitasita kuwachukulia hatua za kisheria mawakala wa pembejeo za ruzuku ambao watakiuka taratibu za mikataba ikiwemo kutopeleka pembejeo kwa wakati ama kutopeleka kabisa.
Akizungumza na ripota wetu ofisini kwake Afisa kilimo, mifugo na ushirika wilaya ya Makete Bi. Marietha Kasongo amesema kwa kuwa kila wakala anayesambaza pembejeo hizo wana mkataba na halmashauri,wanatakiwa kusambaza pembejeo hizo kwa wakati na ambaoa hawatafanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Sheria ziko wazi tu kwa kuwa wakala awe kampuni ama mtu binafsi ana wajibu wa kuhakikisha mbolea ama mbegu zianfika kwa wakati kwa kuwa wakati wa kuwapa mikataba huwa wanaelezwa na wanakubali na ndiyo maana wanasaini”alisema Bi. Kasongo.
Amesema idara yake huwa inachukua hatua papo hapo kwa wakala ambaye analeta usumbufu na hivyo kuwaomba wananchi kwenye maeneo yao kutoa taarifa pale ambapo wakala anachelewa kuwaletea pembejeo kwa wakati ama hakuleta kabisa ili ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria ikiwemo kusitisha mkataba wake na kumtafuta wakala mwingine mapema ili shughuli iendelee.
Bi Kasongo amesema haiwezekani kijiji ama kata kutopata kabisa pembejeo kwa kuwa wagani wa kilimo wapo katika ngazi ya kata hivyo taarifa zinafika mapema wilayani na kutatuliwa kabla ya msimu husika kupita.
Katika hatua nyingine afisa huyo amezungumzia hatua ya serikali kubadili jina la mbolea ya minjingu na kuiita minjingu mazao na kusema lengo la serikali ni kuinua viwanda vya ndani na ikizingatiwa kuwa mbolea hiyo inatengenezwa hapa nchini.
Amesema wananchi wanatakiwa kuitumia mbolea hiyo ambayo inatengenezwa kwenye kiwanda kilichopo Arusha na kwa kuwa mbolea hiyo inapatikana kwa bei nafuu kuliko mbolea nyingine ambazo zinatengenezwa nje ya nchi na kuingizwa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment