HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, April 28, 2013

UKIMWI NI SIFA YA MKOA WA NJOMBE - MKUU WA MKOA WA NJOMBE

Na Edwin Moshi, Makete

Pamoja na mkoa wa Njombe hii leo kuadhimisha miaka 49 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, imeelezwa kuwa mkoa huo ndiyo unaoongoza kitaifa kwa kuwa na maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi ya asilimia 14.8

Kufuatia hali hiyo mkoa huo umejipanga ipasavyo kukabiliana na changamoto hiyo ambayo inaleta sifa mbaya kwa taifa, zoezi litakaloanza mwezi Juni mwaka huu

Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa mkoa wa Njombe Kapteni mstaafu Aseri Msangi ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 49 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kitaifa katika Kata ya Itundu wilayani Makete

Amezitaja sababu zinazopelekea maambukizi ya vvu kuwa juu kuwa ni pamoja na kurithi wajane, wanawake kutokuwa na amri juu ya miili yao hivyo kuogopa kumwambia wanamme kutumia kondomu wakati wa kufanya mapenzi, wanaume kutofanyiwa tohara pamoja na wanaume kuoa wake wengi

“Hata biblia yenyewe inaruhusu tohara, na kwa taarifa yako mwanaume aliyetahiriwa inampunguzia yeye kupata maambukizi ya vvu kwa asilimia 60, lakini bado inashangaza watu hawataki kutahiriwa, sasa unategemea utaponaje kwenye maambukizi” alisema Msangi

Amesema mkoa umejipanga ipasavyo kupunguza maambukizi hayo kwa kuelimisha wanaume kufanyiwa tohara ambapo mwezi Juni hadi Augusti mwaka huu zoezi la tohara litafanywa mkoa mzima huku mkuu huyo wa mkoa akiwa namba moja kuongoza zoezi hilo la uhamasishaji kwenye kila kata ya mkoa wake

Pamoja na hayo mkuu huyo amesisitizia watu kutambua historia ya wapi walipotoka, kutumia wataalamu katika shughuli zao ikiwemo kilimo na ufugaji, ambapo watu wengi hukosa mazao kama walivyokuwa wakitarajia kutokana na kutotumia pembejeo za kisasa za kilimo

“Mtu hadi leo unatumia mbegu za mababu zako halafu utegemee kuvuna gunia 30 kwenye heka moja, hilo suala halipo ng’o wewe fuata wataalamu wa kilimo wakuelekeze namna ya kupanda, kutumia mbolea na namana ya kupalizi na utumie mbegu gani halafu tuone kama hutavuna magunia ya kutosha” alisisitiza Msangi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad