Diwani wa Kata ya Kilangala wilayani Lindi Vijijini Somoe Mwaya akihamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Meneja wa CHF, Constantine Makalla akimsikiliza mmoja wa wananchi waliohudhuria mafunzo hayo.
Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma Grace Kisinga akielekeza kauli mbiu ya NHIF/CHF kwa wananchi, kushoto kwake ni Meneja wa NHIF Mkoa wa Lindi Fortunata Raymond.
Sehemu ya Wananchi waliohudhuria uhamasishaji huo wakionesha ishara ya kukubaliana na CHF.
Kazi ikiendelea, Maofisa wa NHIF wakiendelea kusikiliza ushauri na kutoa ufafanuzi kwa wananchi.
Baada ya kuazimia, wananchi na maofisa walianza kuserebuka ikiwa ni ishara ya Afya bora kwa wote.
Wananchi wakifuatilia mada kwa umakini.
Na Mwandishi Wetu, Lindi
WANANCHI wa Kata ya Kilangala, wilayani Lindi Vijijini wameazimia kwa pamoja kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuondokana na adha ya kutafuta fedha za matibabu wakati wanapougua.
Azimio hilo walilifikia baada ya kuhamasishwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuelezwa umuhimu na faida wanazoweza kupata wakiwa wanachama wa CHF.
Wananchi hao walisema kuwa wako tayari kujiunga na Mfuko huo ambao wanaamini kwa umoja wao watasaidia kuboresha hata huduma za afya ndani ya kata yao kutokana na usimamizi wa fedha za CHF kuwa chini ya mamlaka ya wananchi.
Akizungumza na wananchi hao, Meneja wa CHF, Constantine Makalla, alisema kuwa kujiunga kwa wananchi hao ndani ya Mfuko huo kutaongeza msukumo wa maboresho ya vituo vya kutolea matibabu vinavyozunguka maeneo hayo.
“Jamani ndugu zangu, tunatambua kabisa kuwa ipo changamoto kubwa ya dawa ambayo wengi wenu inawakwamisha kujiunga na CHF, lakini niwaambie tu kwamba hicho kisiwe kikwazo kwani umoja wenu ndio unaweza ukasaidia kudhibiti hata dawa zinazoletwa ndani ya vituo vyenu na fedha za CHF mnaweza kuzitumia kununulia dawa na kufanya maboresho mengine,” alisema Bw. Makalla.
Alisema kuwa mchango anaotakiwa kuuchanga mkuu wa kaya ambao ni sh. 10,000 kwa mwaka utaisadia kaya nzima kupata matibabu bure kwa kipindi hicho.
Naye Diwani wa Kata hiyo, Somoe Mwaya aliuahidi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwa kilichoazimiwa na wananchi hao kitafanyika ili kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Mfuko huo za kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa kwenye Mfumo wa Bima ya Afya.
Aidha aliupongeza Mfuko pamoja na juhudi zinazofanywa na Mama Salma Kikwete za kuwaunganisha akina mama mbalimbali na watoa huduma.
NHIF kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wanaendelea na zoezi la uhamasishaji katika kata mbalimbali mkoani Lindi ambapo zaidi ya wanawake wajasiriamali 600 watafikiwa.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya una mpango maalum wa kuhakikisha unawanyanyua wanawake nchini kote ili waweze kuzisaidia familia zao kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.
No comments:
Post a Comment