Na Edwin Moshi, Makete
Mawasiliano ya barabara ya Makete – Njombe yamekatika tangu jana jioni kufuatia lori lenye namba za usajili T 197 ACR lililokuwa limepeleka nguzo za umeme wilayani Makete kukwama katikati ya barabara eneo la Lwamadovela kata ya Tandala wilayani Makete kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.
Akizungumza na Ripota wa Mtaa kwa Mtaa Blog, dereva wa lori hilo ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema lori lake limekwama kutokana na kumomonyoka kwa udongo uliokuwa ukingoni mwa barabara ambao uliziba nusu ya barabara hali iliyomfanya kuukwepa udongo huo na kupita pembezoni mwa barabara ndipo alipokwama.
Amesema mara baada ya kukwama mvua zilianza kunyesha na kusababisha udongo huo ulioporomokea barabarani kuwa tope zito lililosababisha utelezi barabarani hapo.
“Namshukuru Mungu gari hili limekwama likiwa tayari limeshapakua nguzo za umeme kule wilayani na hapa nilikuwa narudi la sivyo sijui tungelitoaje ama ningetokaje hapa ukizingatia pia hakuna mawasiliano ya simu hapa”alisema dereva huyo.
![]() | ||||
Greda la Halmashauri ya Wilaya ya Makete likiivuta lori hilo. |
Hali hiyo imesababisha magari yanayoingia na kutoka wilayani Makete kushindwa kufika kutokana na lori hilo kufunga barabara na kujikuta yakiishia kupiga kambi eneo hilo kusubiri hatama ya kuondolewa kwa lori hilo.
Ripota wetu ameshuhudia abiria waliokuwa katika magari mbalimbali wakivuka eneo hilo kwa miguu kwenda ng’ambo ya pili kuchukua usafiri mwingine hasa bodaboda ambazo zilikuwa zimepiga kambi eneo hilo hadi Ikonda ambako kuna uafadhali wa kupata usafiri wa kwenda Njombe huku ndugu wa wagonjwa waliokuwa wakienda kupata matibabu kwenye hospitali ya Consolata ikonda wakipata tabu ya kuwasafirisha hadi kwenye hospitali hiyo iliyopo umbali wa zaidi ya kilometa mbili kutoka eneo la tukio.
“kama unayoona mwenyewe broo, huyu mzee wangu anaumwa tena anaumwa miguu, natembea naye taratibu na tukibahatisha usafiri mbele huko itakuwa poa na kama tukikosa ndiyo hivyo tena maana hata tukipata bodaboda itabidi apande yeye mimi nibaki yaani acha tu kaka” alisema Onesmo Mahenge.
Jitihada za kulinasua lori hilo zilifanywa na maafisa wa halmashauri ya wilaya ya makete ambao walikuwa wakielekea mkoani Njombe kikazi wakiongozwa na Afisa Utumishi wa wilaya hiyo Bw. Mwalufunda ambapo walilazimika kupiga simu wilayani kuomba msaada wa greda la halmashauri hiyo kufika eneo la tukio kutoa msaada.

Jitihada hizo zilizaa matunda ambapo greda hilo lilifanikiwa kulivuta na kulinasua lori na hatimaye mawasiliano ya barabara hiyo yakarejea majira ya saa tano na nusu.
Hadi naondoka eneo la tukio magari yalikuwa yakipita kama kawaida lakini ilikuwepo hofu ya udongo kuzidi kuporomoka kama mvua zingezidi kunyesha.
Mtandao huu unashauri wahusika kuangalia haraka namna ya kukomesha hali hiyo ili kuimarisha huduma za wananchi wanaotegemea barabara hiyo
No comments:
Post a Comment