HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 10, 2012

RC DODOMA AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI KUZUNGUMZIA SENSA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi amesema kuwa Viongozi wa Dini wanamchango mkubwa katika kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 26 mwaka huu.

Dr. Nchimbi aliyasema hayo leo hii kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Dodoma alipokutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kwa lengo la kuzungumzia ushiriki wa viongozi hao katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika na kufanikiwa kama lilivyopangwa na serikali.

Dr. Nchimbi alisema kuwa viongozi wa dini wanadhamana kubwa katika nchi yetu kwa kuzingatia kuwa wanawakilisha au kuongoza jamii kubwa nyuma yao na kwa kuwa wao wanauelewa mpana wa suala la Sensa basi ni jambo la busara wakiwasaidia waumini wao pia kupata uelewa sahihi juu ya zoezi la Sensa. Aidha amewataka viongozi hao kwa dhamana walizonazo kwa Mwenyezi Mungu kuliombea Dua Taifa letu na Zoezi zima la Sensa kwani kwa kutoa ushirikiano kama huo zoezi hili litafanikiwa.

Dr. Nchimbi aliongeza kuwa anaamini viongozi hao wa dini ndio wataonesha mfano wa kusimama katika utiifu, uadilifu na unyenyekevu kwa Mungu wao kwa kuhakikisha zoezi la sense linafanyika vizuri. Akizungumzia kuhusu Sensa ya mwaka huu, Dr. Nchimbi alisema kuwa Sensa sio tu kuhesabu idadi ya watu bali ni pamoja na masuala mengine ya msingi kama idadi ya mifugo na shughuli nyinginezo.

Hii itasaidia mipango ya maendeleo na huduma muhimu kutolewa na serikali kulingana na mahitaji halisi, alibainisha Dr. Nchimbi na kuwataka wananchi wote watoe ushirikiano wakizingatia kuwa Sensa ni jukumu na wajibu wa kila mmoja hapa nchini na kuwa taarifa watakazotoa zitabaki kuwa siri na kutumika kwa matumizi yale tu yaliyopangwa kwenye Sensa.

Kwa upande wao viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini Mkoa wa Dodoma wamesema wako tayari kushirikiana na serikali katika kufanikisaha Sensa ya mwaka 2012. Akizungumza kwa niaba ya taasisi ya Dodoma Islamic Development Foundation, Katibu wa taasisi hiyo Alhaj Hussein Janab alisema kuwa viongozi wa dini wako tayari kushiriki zoezi la Sensa na pia wanafanya kazi ya kuhamasisha waamini na wafuasi wao.

Akizungumza kwa niaba ya kanisa la Mennonite Tanzania Kanda ya Kati Mchungaji Chacha Marwa wa kanisa hilo alisema kuwa viongozi wa dini wanawajibu wa kuisaidia serikali kwa kupeleka tarifa sahihi na za kueleweka zinazotolewa. Aliongeza kuwa serikali haina ubaguzi wa aina yeyote ile hivyo ni jukumu la viongozi wa dini nao kupinga aina yoyote ya ubaguzi au kiashiria chochote cha kuleta ubaguzi hasa kwenye mazoezi makubwa kam hili la Sensa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad