Friday, August 24, 2012

grand malt kukabidhi vifaa vya michezo kwa ligi kuu zanzibar kesho


Na Mwandishi Wetu

WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Soka Zanzibar, kinywaji cha Grand Malt kesho wanatarajia kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu zote zitakazoshiriki ligi hiyo.

Akizungumza na ripota wa Mtaa Kwa Mtaa Blog, Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema hafla ya kukabidhi vifaa hivyo itafanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View kuanzia saa 4 asubuhi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk.

Meneja huyo alisema, timu zote 12 zinazoshiriki ligi hiyo zitakabidhiwa vifaa ikiwemo, jezi na mipira kwa ajili ya kufanikisha ushiriki wao.

“Kila kitu kinakwenda sawa na tumepanga kukabidhi vifaa siku hiyo, kwani tunataka tuwe na ligi yenye ushindani mkubwa. “Grand Malt imejitolea kwa kila hali kuhakikisha inakuza michezo Zanzibar na hasa ukichukulia ni muda mrefu ligi yao ilikuwa haina udhamini wa uhakika,” alisema.

Grand Malt, kinywaji kisicho na kilevi ndio ambao wameingia udhamini wa ligi hiyo inayosimamiwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

No comments:

Post a Comment