Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Injinia William Mhando akionyesha moja ya nguzo za umeme zinazotumika kwa uwizi alioubaini katika maeneo mbali mbali ya Jijini Dar.
Fundi wa Tanesco akikata Umeme katika nyumba iliyokuwa ikiiba Umeme.
Mmoja wa wakazi wa nyumba Iliyokuwa ikiiba umeme akitoa maelezo kwa Wakuu wa Tanesco.
WIZI wa umeme kwa njia ya mtandao umemfanya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Injinia William Mhando, kuingia mitaani kushiriki zoezi la ukaguzi wa mita za wateja.
Akiwa kwenye zoezi hilo ambalo kwa wananchi lilionekana si la kawaida kutokana na kufuatana na baadhi ya mameneja na wataalamu Mhando alisema wamepokea taarifa ambazo si nzuri za wizi wa umeme kwa njia ya mtandao hali iliyomlazimu kufuatilia kwa makini tangu ngazi ya chini kabisa.
Mhando alisema tangu kuanza kuzifanyia kazi taarifa hizo wamekamata watu 2 Dodoma na 3 Dar es Salaam ambao kesi zao zimefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutumia umeme ambao haujulikani umenunuliwa wapi.
“Utakuta mteja amenunua umeme wa Sh10’000/ kwetu lakini unapokwenda kukagua utakuta anaumeme wa zaidi ya pesa hizo, nah ii inamaanisha kuna sehemu zingine wananunua tofauti na Tanesco ambapo kwenye mfumo haupo,” Alifafanua Mhando.
Alipoulizwa kuhusu sababu za kuwepo kwa tatizo hilo Mhando alisema tuna wasiwasi kuwa mtaalamu aliyekuja kuingiza mfumo huo aliacha program mtaani na kufanya watu wenye nia mbaya kutumia nafasi hiyo.
Hata hivyo Mhando alisema tatizo hilo limegundulika haraka kutokana na mita maalum (Automatic Meter Reader) zilizofungwa ambazo husomwa moja kwa moja kwenye Tanesco bila ya kwenda kwa mteja na ndio maana tatizo hilo limegundulika haraka.
Aidha alisema wameanza kufunga mfumo mwengine wakudhibiti wizi aina hiyo kwa kufunga kifaa maalum (Supply Group hold) ambacho hadi sasa kimefungwa kwa wateja wakubwa 3000 jijini Dar es Salaam na kudhibiti wizi wa aina hiyo na zoezi hilo litaendelea kwa wateja wakawaida.
Mbali na wizi wa mtandao Mkurugenzi huyo alishuhudia wateja waliojiunganishia umeme kabla haujafika kwenye mita na kuamuru watendaji wake kukata umeme huo huku akiamrisha jeshi la polisi kuwachukua na kuwafungulia mashitaka ya wizi, ambapo mama mwenyenyumba mmoja na Meneja wa Baa ya King Paris walichukuliwa na polisi.
Katika eneo la Keko mbali na nyumba za kawaida umeme ulikatwa kwenye nyumba za wageni pamoja na Baa mbalimbali zikiwemo baa ya Miami Shambwe na Baa ya King Paris zilizopo kwenye eneo hilo.
Nae Meneja wa kanda hiyo ya Temeke Richard Mallamia alisema hasara inayotokana na wizi wa umeme ni zaidi ya Sh80Millioni ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo wamefanikiwa kukusanya Tsh40Millioni kutokana na faini pamoja na ukusanyaji wa madeni.
Zoezi hilo ambalo ni endelevu linatarajia kukamata watu zaidi ili kuweza kufidia hasara ambayo shirika linapata kutokana na wizi.
Tanesco hukusanya mapato mengi zaidi ya 80% kutoka kwa watumiaji wakubwa waumeme ambao ni 20% ya wateja wote na ndio sehemu waliyoanza kufanya udhibiti wa ufungaji wa vifaa maalum vya kuzuia wizi.


No comments:
Post a Comment