Friday, July 20, 2012

KELVIN YONDANI NI HALALI KUWA MCHEZAJI WA YANGA:UAMUZI WA KAMATI YA SHERIA TFF

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji (ambayo katika uamuzi huu itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai 17 mwaka huu, baada ya kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika mashindano ya Kombe la Kagame kama zilivyowasilishwa mbele yake imefikia uamuzi ufuatao;

1. Kwa mujibu wa mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu, Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji kama Sekretarieti ilivyofanya katika barua yake ya Julai 14 mwaka huu ulikuwa sahihi.

2. Kamati ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.

3. Aidha Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho la kisheria haupo.

4. Hata kama kamati ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu.

5. Kisheria utata huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati akiwa huru.

Kutokana na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012.

Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

2 comments:

  1. hongera sana mgongolwa.mkataba wa simba ni wa kugushi,uliandaliwa haraka haraka kiujanjajanja na matokeo yake ndio hayo ya makosa ya kijinga.hivi inawezekana vipi mkataba usainiwe desemba 2011 halafu makosa ya kiuandishi yabainike baada ya miezi saba?wakati Rage anapiga kelele za kushitaki fifa kumbe hakuwa ameuona hata mkataba aliokuwa anautetea?ndio matatizo ya kuandaa mkataba wa mwaka 2011 ndani ya mwaka 2012 lazima kuna sehemu utajisahau.kugushi kwa namana hii kulitukotukosesha kushiriki fainali za u-20 mwaka 2005 hivyo tukomeshe tabia hizi. wenye mambo haya ya kugushi wasipewe nafasi tena kwenye soka.umefika wakati kwa viongozi wa simba wawe majasiri kuwaambia ukweli wanachama wao wanapokosea badala ya kutaka kuwasukumia watu wengine lawama na wao kusubiri kusifiwa tu.kwa jinsi wanavyopenda sifa kama kweli walimsajili yondani desemba 2011 lazima wangetutangazia na kutamba kwenye vyombo vya habari

    ReplyDelete