Mchezaji kutoka Chuo cha St.John cha Dodoma, Obiara Anyoti akicheza dhidi ya mpinzani wake Kweka John (hayupo pichani) wakati wa mashindano ya Safari Higher Learning Pool Competition yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Mchezaji kutoka Chuo cha MUCCOBS CHA Mkoani Moshi, Kweka John akicheza dhidi ya mpinzani wake Obiara Anyoti(hayupo pichani) wakati wa mashindano ya Safari Higher Learning Pool Competition yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Wachezaji wakishindana kulagi wakati wa mashindano ya Safari Higher Learning Pool Competition yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Wachezaji wakishindana kulagi wakati wa mashindano ya Safari Higher Learning Pool Competition yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Wanafunzi wachezaji kutoka vyuo mbalimbali shiriki wa mashindano ya Safari Higher Learning wakifuatilia mashindano yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Wachezaji wa chuo cha MUCCOBS cha Moshi wakipanga namna ya kufanya mashambulizi wakati wa mashindano ya Safari Higher Learning Pool Competition yaliyofunguliwa rasmi jana Mkoani Iringa.
Na Mwandishi Wetu,Iringa
AFISA Utamaduni Manispaa ya Iringa,Carlos Mbinga amewataka Watanzania kuupokea mchezo wa pool kwa mikono miwili kutokana kwamba hivi sasa umekuwa ni sehemu ya ajira kwa vijana na hivyo kufuta zana ya kuwa ni mchezo wa kihuni.
Mbinga aliyasema hayo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa fainali za taifa za mashindano ya pool kwa wanafunzi wa vyuo vikuuu vinane kutoka katika mikoa minane ya Tanzania Bara.
Mbinga ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa katika ufunguzi huo wa mashindano hayo yanayodhaminiwa na wadhamini wakuu wa mchezo wa pool nchini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, alisema kuwa mchezo wa pool ni kati ya michezo ambayo kwa hivi sasa inatakiwa kuungwa mkono na Watanzania wote.
Alisema kuwa wana kila sababu ya kujivunia kwa wadhamini wa mchezo huo bia ya Safari Lager kuamua kuleta fainali hizo mkoani hapa kutokana kwamba ujio huo umeweza kuongeza kipato kupitia kwenye biashara mbalimbali zinazofanyika.
"Napenda kuwashukuru Safari Lager kwa kuweza kuleta fainali hizi mkoani hapa kutokana na kwamba wafanyabiashara mbalimbali wameweza kujiongezea kipato kupitia fainali hizi,"alisema Mbinga.
Naye mwenyekiri wa chama cha mchezo wa pool Tanzania (TAPA) Fredy Mushi alisema kuwa kila mwaka mashindano hayo yanazidi kukua zaidi kutokana na uwezo unaoonyeshwa na wachezaji wa vyuo vyote.
Mushi alisema kuwa kila mwaka unaonyesha kuwa na mabadiliko makubwa katika mashindano hayo kutokana na kila chuo kuonekana kujiandaa vizuri na hivyo upinzani kuzidi kuongezeka.
"Ninavyoona upinzani wa fainali za mwaka huu kwa wachezaji kuonyesha viwango vya kutisha, mabingwa watetezi chuo cha IFM kutokana Dar es salaam wazitegemee mteremko maana kila chuo kinaonekana kujiandaa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo,.'alisema Mushi.
Mratibu wa fainali hizo, Peter Zacharia (Kosovo), alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya fainali hizo yameenda vizuri ikiwemo usafiri, malazi na kila kitu kinachohusiana na fmashindano.
Zacharia alisema kuwa timu zote zimewasili mkoani hapa bila matatizo yoyote na kupokelewa na mamia ya wakazi wa Iringa kwa furaha na nderemo.
Fainali hizo zinashirikisha vyuo vikuu vinane ambavyo vilifanikiwa kuwa mabingwa kwenye mikoa yao katika ngazi ya mikoa ya mashindano hayo.
Vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na mikoa vinakotoka ikiwa kwenye mabano kuwa ni mabingwa watetezi IFM (Dar es Salaam), RUCO (Iringa), TIA (Mbeya), IAA (Arusha),St John's (Dodoma),MUCCOBS (Kilimanjaro),St Agustine (Mwanza) na Mzumbe (Morogoro).
Bingwa wa fainali hizo kwa timu ataondoka na kitita cha fedha taslim Sh.Mil.2.5, mshindi wa pili Sh.Mil.1.5, mshindi wa tatu Sh.Mil.1.3 na mshindi wa nne Sh.Mil.1.
Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wanaume bingwa atazawadiwa Sh.300,000, mshindi wa pili Sh.200,000, mshindi wa tatu Sh.150,000 na mshindi wa nne Sh.100,000.
Kwa upande wa wanawake bingwa atajizolea Sh.200,000, mshindi wa pili Sh.150,000, mshindi wa tatu Sh.100,000 na mshindi wa nne Sh.50,000.
Mashindano hayo yanatarajia kufikia kilele chake kesho ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi.

No comments:
Post a Comment