Afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya simu Tanzania(TTCL) Said Amir Said(katikati)akikabidhi zawadi za siku kuu ya Eid kwa mlezi wa kituo cha watoto yatima cha Alhuda Bw Yahaya Karebile.(kulia).
Afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya simu Tanzania(TTCL) Said Amir Said akikabidhi zawadi za siku kuu ya Eid kwa watoto Mustapher Robert na Suleiman wa kituo cha watoto yatima cha Mkombozi.
Afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya simu Tanzania(TTCL) Said Amir Saidakikabidhi zawadi za siku kuu ya Eid kwa mlezi wa kituo cha wazee wasiojiweza cha Njoro Bi Ndeta Tenga.
Wafanyakazi wa TTCL mkoa wa Kilimanjaro wakiwa na wageni mbalimbali katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi za siku kuu ya Eid kwa watoto yatima na wazee wasiojiweza.
Na Dixon Busagaga,Moshi.
KAMPUNI ya simu Tanzania (TTCL), imetoa zawadi ya vyakula kwa ajili ya watoto yatima, walemavu na wazee wasiojiweza, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mipango ya kampuni hiyo, yenye lengo la kusaidia makundi maalum ya kijamii.
Msaada huo ikiwemo sukari, mchele, mafuta ya kupikia, unga na sabuni vyenye thamani ya shilingi milioni 1.6, ulitolewa juzi kwa walengwa hao wanaolelewa kwenye vituo vya Mkombozi, Alhuda Fund Centre na kikundi cha wazee wasiojiweza kilichopo kata ya Njoro mjini Moshi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, afisa mtendaji mkuu wa TTCL Said Amir Said, alisema kampuni hiyo inatambua mahitaji muhimu ya kijamii kwa makundi maalum, na kuongeza kuwa msaada huo ni moja ya utekelezaji wa mpango wa kuyasaidia makundi hayo.
Said aliongeza kuwa licha ya msaada huo kuwa sehemu ya kuungana na makundi hayo ya kijamii katika kusherehekea sikukuu ya Eid el Fitr,pia kampuni hiyo imeelekeza nguvu katika kujali matatizo ya watu kwenye makundi hayo na kutafuta njia za kuwasaidia.
“Sisi TTCL kama kampuni ya umma na ya kizalendo, tunajali sana jamii inayotuzunguka pamoja na matatizo yake, ndio maana leo tunatoa msaada huu wa vyakula kwa makundi haya ya wahitaji, tukijua kuwa ni jukumu letu kama kampuni ya Kitanzania kusaidia”, alisema afisa huyo.
Pia alisema kampuni yake itaendelea kuihudumia jamii, ambapo sehemu ya mapato yake itaelekezwa kutoa huduma za kijamii, kama hatua mojawapo ya kuonyesha kuwa sehemu ya mapato hayo inarejeshwa kwa jamii.
Msaada huo wa chakula ni sehemu ya misaada mingine iliyotolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, visiwani Zanzibar ukiwemo mkoa wa Kilimanjaro, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10, katika kusherehekea sikukuu ya Eid.
No comments:
Post a Comment