HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, June 5, 2011

Waziri Mkuu afunga kilele cha Siku ya Mazingira Duniani mkoani Ruvuma

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
Na Riziki Abraham- Ruvuma

Wananchi wametakiwa kuepuka tabia ya kukata miti, kufyeka misitu ovyo, kuacha uchomaji moto misitu na uoto wa asili, na badala yake waone umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya ardhi ili kukabiliana na ukame na kuenea kwa hali ya jangwa, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda amesema hayo leo katika kilele cha Siku ya Mazingira duniani mkoani Ruvuma alipokuwa akihutubia wananchi wakati wa kufunga maadhimisho hayo ambapo kwa niaba yake aliwakilishwa na Waziri wa Nyumba na Mendeleo ya Makazi Mhe. Prof. Anna Tibaijuka.

“nasema ingawa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yanalenga zaidi masuala ya misitu, ni vyema tunapoadhimisha, tukumbushane pia suala la usafi wa mazingira wa miji na maeneo yetu maana hali ya miji katika baadhi ya maeneo tunamoishi hairidhishi kutokana na mirundikano ya taka ngumu na kutiririka kwa majitaka” alisema Waziri.

Sambamba na hilo Waziri Mkuu amewakumbusha wananchi juu ya kuendelea na kampeni ya usafi kila siku ya jumamosi ya kwanza ya mwezi kama ilivyozinduliwa na Makamu wa Rais mnamo tarehe 12 februari mwaka huu kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuwa na tabia ya kufanya usafi wa mara kwa mara katika maeneo yanayowazunguka.

Waziri Mkuu amesema kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira inahitaji juhudi za vyombo mbalimbali katika ngazi zote na kwakuwa Serikali za Mitaa zimeunda Kamati za Mazingira ambazo ni kiungo muhimu katika kufikia malengo ya kuhifadhi Mazingira, hivyo ni vyema Kamati hizo zikatumiwa kikamilifu.

Pinda amewataka wananchi kushirikiana na serikali katika kutekeleza sheria na kanuni za hifadhi ya mazingira kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa, kwa kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi, kuendeleza mafanikio yaliyokwisha patikana kwa kusimamia ipasavyo sheria zinazohusika na kuimarisha doria ikiwa ni pamoja na kudumisha utamaduni ulioanza wa kupanda miti, kuhifadhi misitu na uoto wa asili.

Aidha, mgeni rasmi alipata nafasi ya kutoa zawadi kwa Washindi wa usafi wa Mazingira kuanzia ngazi Halmashauri za jiji, Halmashauri za Manispaa, Halmashauri za miji na Halmashauri za Wilaya ambapo Halmashauri ya jiji la Mwanza ndio iliyoongoza ikifuatiwa na Manispaa ya mji wa Moshi, Arusha, Iringa. Pamoja na hao pia Halmashauri ya mji wa Mpanda na Njombe zimepata zawadi na katika ngazi ya Wilaya mshindi ni Halmashauri ya Njombe, Meru na Rungwe ndio walioibuka kidedea na washiriki wengine wakiambulia vyeti vya ushiriki.

Pia Waziri Mkuu amevipongeza Vyombo vya Habari kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuelimisha na kuhamasisha jamii na vilevile aliushukuru Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho ya mwaka huu.

Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Dkt. Terezya Huvisa amewataka wafanyabiashara ndogondogo nchini kuacha kufanya biashara katika maeneo ya kandokando ya barabara kwani ni maeneo hatarishi kwa maisha yao na pia ni uchafuzi wa mazingira, amesema ni vyema wakatii agizo hilo maana mara nyingi wamekuwa wepesi wa kulalamika pindi inapotokea ajali.

Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani kimataifa mwaka huu yamefanyika katika miji ya Mumbai na Delhi nchini India na kitaifa yameazimishwa mjini Songea mkoani Ruvuma, yakienda sambamba na

Maadhimisho ya miaka ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kama njia mojawapo ya kutathimini tulikotoka, tuliko na tunakokwenda.

Uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara umeanza kuazimishwa rasmi na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo utaratibu wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru utaendelezwa na kila Wizara, Mikoa na Taasisi zake zote nchini hadi yatakapofikia kilele chake tarehe 9 Desemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad