Ufunguzi wa wodi mpya ya saratani ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Watoto ni hatua kubwa kwa kuzingatia upatikanaji wa vifaa muhimu kwa matibabu ya watoto waliogundulika na matatizo ya saratani za aina mbalimbali.
Akiongelea ufunguzi huu wa wodi mpya, Dk. Trish Scanlan ambaye ni mtaalamu wa saratani za watoto kutoka Kituo cha Saratani cha Ocean Road, ambako watoto hao ndiko waliko kwa sasa, alisema wodi hii mpya imejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa .
“Watoto wenye matatizo ya saratani wanahitaji kuhifadhiwa katika wodi kubwa ya watoto yenye nafasi ya kutosha na yenye hifadhi ya damu kwa masaa 24, Kitengo cha Watu Mahututi, pamoja na mengine pawe na huduma muhimu ya upasuaji. Vyote hivi vipo katika wodi hii mpua iliyofunguliwa hapa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili”.
Aliongeza kuwa wodi hii mpya imejengwa kwa msaada wa wafadhili mbalimbali wa kimataifa na wa hapa nyumbani ikiwemo taasisi kama ya Love, Hope, Strength Foundation na Children in Crossfire. “Kituo hiki kisingekuwa hapa kilipo bila ya msaada wa marafiki wa Kituo hiki cha Saratani kama vile Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya Children, Bw. Matthew Banks ambaye ndiye msimamizi wa mradi huu, Wizara ya Afya nchini Tanzania, Mtandao wa Kimataifa cha Uchunguzi na Matibabu ya Saratani, watu kadhaa wenye nia njema hapa nchini, pamoja na Mwanzilishi wa Mfuko ‘Love Hope Strength Foundation’ ambaye pia aliugua mara mbili na kupona ugonjwa wa Saratani ya Damu, Bw. Mike Peters –ambaye pia ni mwimbaji wa kundi liitwalo ‘The Alarm’ kutoka nchini Wales”.
Tangu aanze kupambana na ugonjwa wa Saratani ya Damu miaka kadhaa iliyopita, Mike na kundi lake wamekuwa wakizunguka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watu wenye matatizo ya saratani hasa walio katika nchi masikini zaidi duniani. Mfuko huu pia ulitoa pesa kwa ajili ya kufanyia matengenezo wodi 2 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na kwa kuongezea Mfuko huu umedhamiria kukusanya Dola 5,000 za Kimarekani ambazo ni sawa na shilingi. 7.5milioni kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu katika kipindi cha mwezi huu wa Februari ili kusaidia watoto hawa wenye saratani.
Mfuko wa The Love, Hope, Strength kupitia tovuti yao www.lovehopestrength.org umetoa habari kwa umma kuelezea ufunguzi wa kituo hiki cha watoto. Wodi hii ya watoto imepewa jina la ‘Wodi ya Tumaini, Upendo, Ujasiri’.
Kituo cha Saratani cha Ocean Road hivi sasa kinatunza zaidi ya watoto 500 kila mwaka (ikiwa ni zaidi wagonjwa 300 zaidi) kutoka sehemu mbalimbali nchini. Tangu mwezi Novemba 2007, serikali ilitangaza kutoa matibabu bure kwa watu wenye matatizo ya saratani.
Kutokana na huduma hii ya saratani kutolewa bure, idadi ya watu waliopona imeongezeka kutoka asilimia 15-20% mwaka 2006 mpaka 60% (kwa kipindi cha mwaka mmoja) mwaka 2009, hii ikiwa ni mafanikio makubwa kupatikana katika kipindi kifupi cha miaka 3.

No comments:
Post a Comment