HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 27, 2010

elimu inayotolewa kuhusu upigaji kura katika uchaguzi mkuu,izingatiwe - mama Salma Kikwete

Mama Salma Kikwete.

==== ==== ==== =====

NA MWANDISHI MAALUM, IRINGA

MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete, amewataka wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kuzingatia elimu inayotolewa kuhusu upigaji kura katika uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekuwa ikitoa elimu hiyo ili kila mpigakura afahamu anachopaswa kufanya wakati wa kupiga kura hivyo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na UWT wanapaswa kuzingatia maelekezo hayo.

Alisema hayo Oktoba 26, 2010 alipozungumza na wanachama wa UWT katika mikutano ya ndani ya kuwahamasisha kina mama kujitokeza kwa wingi kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Katika mikutano hiyo iliyofanyika katika majimbo ya Njombe Magharibi, Njombe Kaskazini, Njombe Kusini, Kalenga, Mufindi Kusini na Iringa Mjini, Mama Salma Kikwete alisema kura ina thamani na kila mpiga kura anapaswa kuipiga kwa usahihi.

“Zimebaki siku chache tupige kura tafadhali tuzingatie maelezo yanayotolewa ya namna tunavyotakiwa kupiga kura. Kura ni kitu cha thamani usikubali kupoteza kura yako kwa kusababisha iharibike,” alisema Mama Salma.

Katika hatua nyingine aliwataka kina mama wasihadaiwe na kuwapa watu wengine shahada zao za kupigia kura, pia ni kinyume cha sheria kwa mtu kumnyang’anya mwenzake kitambulisho hicho.

Alisema hivyo kufuatia taarifa kwamba kuna baadhi ya kina mama wamekuwa wakinyang’anywa shahada hizo ili wasishiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

Mama Salma ambaye amekuwa akizunguka nchini kote kukiombea kura Chama Cha Mapinduzi, alisema ana uhakika CCM itashinda katika uchaguzi huo, ila kinachotakiwa ni ushindi wa kishindo.

“Tunataka kura zetu zijae mpaka zimwagike, sina wasiwasi wa ushindi hata kidogo,” alisema na kupigiwa kofi na kina mama hao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad