Na Mwandishi Wetu, Moshi
KAMPUNI ya OIKO Credit inayojishughulisha na ukopeshaji fedha kwa taasisi mbalimbali duniani zikiwemo benki, imezikopesha jumla ya shilingi bilioni 2.1/- YWCA Moshi na Saccos ya Wazalendo ili zitumike kuiwezesha jamii ya watu wa kipato cha chini.
Fedha hizo zinazotumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la makao makuu ya YWCA Moshi na uwezeshaji jamii ili ijiendeleze kimaisha kupitia Wazalendo ni muendelezo wa mikopo kutoka kampuni hiyo iliyoitoa katika kipindi cha mwaka huu kwa taasisi 12 nchini unaofikia jumla ya bilioni 8.2/-
Akizungumza jana mjini hapa wakati wa hafla ya kukabidhi hundi Meneja wa Oiko Credit Tanzania Deus Manyeye alisema kuwa lengo la kampuni yake ni kuwekeza kwenye taasisi za fedha zilizolenga kuiendeleza jamii ya kipato cha chini duniani.
Akifafanua Manyeye alibainisha kwamba licha ya kupokea maombi mengi lakini wamehakikisha fedha wanazotoa zinaelekezwa kwenda kusaidia miradi ya uzalishaji inayolenga watu wa hali duni wanaopigania kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
“Tulichunguza na kubaini kwamba YWCA Moshi na Wazalendo Saccos wamekidhi vigezo vya kupewa mikopo kwani walikuwa na nia ya dhati ya kuikomboa jamii ya chini kutoka kwenye umaskini unaoikabili. Tayari fedha zimeshaanza kutumika kama mnavyoona ukarabati wa jengo hili unavyoendelea,” alisema Manyeye.
Aidha kwa kuwa idadi ya watu Tanzania ni kubwa kuliko ile ya Kenya na Uganda taasisi hiyo imepanga kuziwezesha kwa kuzikopesha zaidi asasi na wadau wa nchini ili waweze kuhudumia kundi kubwa la watu kuliko ilivyo sasa ambapo nchi hizo zimekuwa zikipata fungu kubwa la fedha.
Kwa upande wake Katibu wa YWCA, Frida Mbowe alisema kwamba kwa kuwa manispaa hiyo inajiandaa kuwa hadhi ya jiji mkopo huo wa milioni 500/- utawawezesha kukarabati jengo kuwa lenye muundo wa kisasa utakaotoa mvuto kwa wawekezaji kupangisha na kufungua ofisi mbalimbali.
Naye Mbonea Maghimbi ambaye ni mwenyekiti wa Wazalendo aliishukuru Oiko Credit kuwakopesha bilioni 1.6/- na kusema watazitumia kama ilivyokusudiwa kwa kuwawezesha watu wa kipato cha chini kuweza kuinua hali yao kimaisha.
“Mbali na hilo pia tumepanga kuzitumia fedha hizo kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuhifadhi ama kujiunga na Saccos ya Wazalendo na faida mbalimbali watakazonufaika nazo mara watakapotimiza vigezo,” alisema Maghimbi.
Tangu Oiko Credit yenye makao makuu yake nchini Uholanzi ilipoanzishwa nchini mwaka 2006 imejiongezea wateja kutoka sekta mbalimbali ikiwemo benki, SME’s, Saccos, Makanisa na kuwekeza kutoka milioni 260/- hadi kufikia bilioni 16 Juni mwaka huu kutoka wateja wawili hadi 21.
No comments:
Post a Comment