KAMPUNI ya RBP Oil & Industrial Technology (Tz) Limited imetoa kiasi cha sh. milioni tano (5) kwa taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Mitindo House (TMH) kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo cha michezo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kilichopo Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika hafla ya kutoa msaada huo iliyofanyika kwenye hoteli ya Movenpic,Rais wa kampuni hiyo,Mama Rahma Al Kharoosi alisema ameamua kuisaidia taasisi hiyo ili kutoa nafasi kwa watoto hao kuwa na sehemu ya pamoja na kufurahi.
Alisema watu wenye uwezo hawanabudi pia kuwasaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu ama watoto yatima ili kuwafanya wajisikie kama wengine kwani kutoa ni wito na hivyo kwa wale watu wenye uwezo wajitoe kuwasaidia wale wasiojiweza.
Naye mwenyekiti wa TMH ambayo inaundwa na wabunifu wa mitindo,Khadija Mwanamboka alishukuru kwa msaada huo na kusema utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema kituo hicho kitazinduliwa rasmi juni 12 mwaka huu ambapo kitakuwa kikitumiwa na watoto toka vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Ikumbukwe kuwa THM inasimamia kituo cha kulelea watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi kilichopo Magomeni Mikumi ambapo mpaka sasa kina watoto kumi.
No comments:
Post a Comment