===============================
na mwandishi maalumu,
Mwanza
Timu za Kagera na Shinyanga zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya kutofungana wakati wa mechi ya ufunguzi ya Mashindano ya Kombe la Taifa la Kilimanjaro 'Kili Taifa Cup' , kanda ya ziwa iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa leo.
Mechi hiyo ilikuwa ya kusisimua kutokana na kila timu kuonesha kupania kushinda huku wachezaji nguli wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania wakikabilaiana na upinzani kutoka kwa vijana ambao bado hajakuwa na uzoefu katika mashindano.
Mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake huku magoli ya wazi yakishuhudiwa kukosekana katika kipindi hicho.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa kila timu huku madhambi yakitawala na kupelekea mwamuzi wa mchezo huo kutoa kadi ya njano kwa Hamim Abdul baada ya kumfanyia madhambi Victor Issack wa Shinyanga.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada mechi hiyo makocha wa timu zote wamesema kuwa mechi ilikuwa ni ngumu kwa kila upande kutokana na maandalizi mazuri ya wachezaji pamoja na ari waliyonayo.
Hata hivyo kocha msaidizi wa Kagera, Mrage Kabange alisema kuwa wachezaji wake wengi ambao ni vijana na ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano makubwa kama haya wameonesha uhai jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zijazo.
"Vijana wetu ni wadogo, ndio mara yao ya kwanza kushiriki mashindano kama haya." Alisema.
Kwa upande wake kocha Jumanne Ntambi wa Shinyanga alisema kuwa tatizo la ushambuliaji kwa timu yake limempa changamoto ya kulishughulikia ili nao waeze kufanya vizuri katika mechi zinazofuata.
Mechi iliyofuata ilikuwa ni kati ya Mwanza na Tabora ambayo ilichezwa saa kumi alasiri.
No comments:
Post a Comment