HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 26, 2009

I.G.P Mwema Afanya Mabadiliko Madogo Kwa Makamanda Wa Mikoa

Na Mohammed Rama Mhina,
wa Jeshi la Polisi

MKUU wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema amefanya mabadiliko madogo kwa makamanda wa polisi na wakuu wa upelelezi wa mikoa kadhaa.

Msemaji mkuu wa polisi, Kamishna Abdallah Msika alisema jana kuwa katika mabadiliko hayo, IGP Mwema amewateua makamanda wawili wapya wa mikoa na wakuu wawili wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mikoa.

Kamanda Msika aliwataja makamanda wapya kuwa ni Kamishna Msaidizi Stiven Buyuya, ambaye alikuwa afisa mnadhimu wa mkoa wa Mara na ambaye sasa anakuwa kamanda mpya wa mkoa wa Mtwara na Kamishna Msaidizi Augustine Olomi, ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Mwanza ambaye sasa anakuwa kamanda mpya wa mkoa wa Kusini Unguja.

Wengine ni Mrakibu Mwandamizi, Deusdedit Msimike aliyekuwa afisa mnadhimu mkoa wa Arusha na ambaye sasa ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa upelelezi mkoani Mwanza na Mrakibu Joseph Konyo kutoka makao makuu ya upelelezi ambaye anakwenda Kigoma kuwa mkuu wa upelelezi.

Kamanda Msika alisema kuwa mkuu wa upelelezi mkoani Kigoma, Mrakibu Mwandamizi Nsato Marijani amehamishiwa mkoa wa Pwani kuchukua nafasi ya Mrakibu Mwandamizi Gabriel Njau ambaye amehamishiwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Alisema Makamanda waliobadilishwa na kupangiwa vituo vipya vya kazi ni wa mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Robert Mikomangwa ambaye anakwenda mkoa wa Mara kuchukua nafasi ya ACP Liberatus Lyimo aliyehamishiwa mkoani Tabora kuchukua nafasi ya Kamanda ACP Emson Mmari ambaye amehamishiwa makao makuu ya Idara ya Upelelezi jijini Dar es Salaam.

Pia, kwa mujibu wa Msika, kamanda wa Kusini Unguja, ACP Rashid Seifu amehamishiwa makao makuu ya polisi kusaidiana na Naibu Kamishna Venance Tossi katika kikosi cha Operesheni Maalum.

Katika hatua nyingine, kamanda Mwema, amewaagiza wakuu wa vyuo vya polisi kuhakikisha kuwa wanafanya tafiti mbalimbali na kurekebisha mitaala ili askari wanaomaliza mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kujiendeleza na yale ya awali wawe na uelewa wa makosa mbalimbali.

IGP Mwema alitoa maagizo hayo, leo wakati akizungumza na wakuu wa vyuo vya polisi vya Moshi, Zanzibar, Dar es Salaam na Kidatu mkoani Morogoro waliokutana jijini Dar es Saaam.

Katika mkutano huo uliohudhuliwa na Kamishna Clodwig Mtweve, Kamishna Paul Chagonja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai nchini, Kamishina Robert Manumba, IGP Mwema alisema kuwa ili vyuo hivyo viweze kuwa na uwezo kitaaluma ni lazima kufanya utafiti mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad