
Na Claud Mshana,Mwananchi
WAFANYAKAZI WA kampuni ya Mwananchi Communicastions Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya THE CITIZEN, MWANANCHI na MWANASPOTI jana jioni waligubikwa na giza nene baada ya kusikia taarifa za kifo cha mfanyakazi mwenzao, Junitha Makafu(25)(pichani) aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa baada ya kugongwa na gari jijini Dar es Salaam.
Junitha, 25 aligongwa na gari karibu na Kanisa la Full Bible Gospel Fellowship, Mwenge siku ya Jumapili jioni akiwa na mdogo wake pamoja na rafiki yake.
Marehemu, msichana mwembamba aliyejaa kila aina ya staha na tabasamu kwa watu mbalimbali alikuwa mwandishi wa gazeti la The Citizen, gazeti dada la Mwananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Sam Sholei alikielezea kifo hicho kuwa ni cha kushitusha na kusikitisha.
Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Citizen, Bakari Machumu alisema Junitha alikuwa rafiki, anayejiheshimu na mwenye nia ya kujifunza na kuongeza kuwa tumempoteza akiwa mwanzo kabisa wa kazi yake ya uandishi wa habari.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya utawala ya MCL ilisema, msiba upo nyumbani kwao Kigamboni jijini hapa.
Alijiunga na gazeti la The Citizen, Juni Mosi mwaka huu baada ya kumaliza mafunzo ya mwaka mmoja chini ya mpango wa MCL wa kukuza waandishi mjini Nairobi, Kenya. Alihitimu shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma katika Chuo Kikuu cha St Augustine (Saut), mjini Mwanza.
Akiwa na gazeti la The Citizen alikuwa mwandishi wa habari, makala na alikuwa na matarajio ya kuwa Mhariri Mkuu wa habari ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo .
Kwa mujibu wa uchunguzi wa madaktari, Junitha alipata majeraha ya ndani ya tumbo jambo lililowalazimu madakari kuondoa kidole tumbo walipomfanyia upasuaji siku ya Jumapili.
Dada wa marehemu, Dk Cecilia Makafu alisema siku ya tukio , mdogo wake alikuwa na rafiki yake Magdalena Msenga na mdogo wao Tobieta Makafu, ambapo Magdalena alivunjika mkono wakati gari lililokuwa katika mwendo wa kasi lilipowagonga.
Dk Cecilia alisema kuwa mashahidi wa ajali hiyo walisema dereva alikuwa katika mwendo wa kasi na kupoteza mwelekeo ndipo alipowagonga.
wakiwa nje ya barabara ya Sam Nujoma.
Mungu aiweke mahali pema roho ya Junitha.
-AMEEN
No comments:
Post a Comment