Sunday, June 21, 2026

RC SHIGELA: UJENZI WA UWANJA WA MAGOGO KUANZA KABLA YA JULAI 6


Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema mkandarasi wa ujenzi wa Uwanja wa Magogo unaotarajiwa kutumiwa na timu ya Geita Gold FC atakabidhiwa eneo la mradi kabla ya Julai 6, 2026, ili kuanza kazi ya ujenzi inayotarajiwa kukamilika ndani ya msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2026/2027.

Shigela ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa kwa ajili ya kuipongeza Geita Gold FC baada ya kutwaa ubingwa wa Championship na kufuzu kurejea Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

"mimi nimewaita na kuwashirikisha viongozi wa timu,manispaa ya Geita pamoja na mbunge tumekubaliana kutenga Shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Nyankumbu, ili timu hiyo iendelee kuutumia katika kipindi cha mpito wakati ujenzi wa Uwanja wa Magogo ukiendelea.

Shigela pia amewataka viongozi wa Geita Gold FC na Manispaa ya Geita kuhakikisha wanafanya usajili wa wachezaji wenye uwezo na ushindani wa hali ya juu ili timu hiyo iweze kuhimili ushindani wa Ligi Kuu na kuwakilisha vyema Mkoa wa Geita.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Zubeir Katwira, amesema mafanikio ya timu hiyo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa klabu, Halmashauri ya Manispaa ya Geita, wadhamini na mashabiki waliokuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha msimu.

Katwira amesema msaada na mazingira mazuri yaliyowekwa na viongozi yameiwezesha timu kutimiza malengo yake ya kutwaa ubingwa wa Championship na kurejea Ligi Kuu ya NBC.

Geita Gold FC imehitimisha msimu wa Championship ikiwa kileleni mwa msimamo kwa kukusanya pointi 77, na hivyo kutwaa ubingwa wa ligi hiyo pamoja na kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara katika msimu wa 2026/2027.

Mkuu wa MKOA WA GEITA,Martine Shigela ametoa zawadi ya kiasi cha Shilingi Milioni 40 kwa ajili ya kuipongeza timu hiyo. 

No comments:

Post a Comment