Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeeleza kuwa uzalishaji wa pareto nchini bado haujakidhi mahitaji ya viwanda vya ndani, huku Tanzania ikizalisha wastani wa tani 4,000 za maua makavu kwa mwaka dhidi ya mahitaji ya tani 9,000, hali hiyo imeacha upungufu wa tani 5,000, sawa na zaidi ya nusu ya mahitaji yaliyopo.Akizungumza Juni 20, 2026, katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Kilimo Mwandamizi wa COPRA, Sikitu Mwakeja, alisema kuna fursa kubwa kwa wakulima, vijana na wawekezaji wa sekta binafsi kuingia katika kilimo cha pareto kutokana na soko la uhakika lililopo nchini.
Mwakeja alibainisha kuwa bei ya maua makavu ya pareto imeendelea kuwa ya kuvutia, ikifikia kati ya Sh4,000 na Sh5,000 kwa kilogramu kulingana na kiwango cha ubora, ameongeza kuwa kwa kufuata mbinu bora za kilimo, ekari moja inaweza kutoa hadi kilogramu 500 za maua makavu kwa msimu, hivyo kulifanya zao hilo kuwa miongoni mwa mazao yenye tija kwa wakulima.
Kwa sasa, uzalishaji mkubwa wa pareto unafanyika katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, COPRA imewahimiza wadau mbalimbali kutumia fursa ya mahitaji makubwa yaliyopo sokoni ili kuongeza uzalishaji, kupunguza pengo lililopo na kuimarisha mchango wa zao hilo katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia mnyororo wake wa thamani.
No comments:
Post a Comment