Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua muhimu katika kuimarisha matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia kufuatia ziara ya siku mbili ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Najat Kassim Mohammed nchini India.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kitaasisi kati ya Tanzania na India, hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za maendeleo katika sekta mbalimbali zinazotumia teknolojia ya nyuklia.
Maeneo ya kipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya saratani, uhifadhi wa chakula kwa teknolojia ya mionzi, pamoja na tafiti za kisayansi na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani.
Kupitia makubaliano hayo, vijana wa Kitanzania wanatarajiwa kunufaika na nafasi za mafunzo ya muda mfupi na mrefu nchini India, jambo litakalosaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa nyuklia na kuimarisha ujuzi wa kisasa nchini.
Katika ziara hiyo, Profesa Najat alitembelea taasisi mbalimbali zikiwemo BRIT, Idara ya Teknolojia ya Nyuklia ya India pamoja na Tata Memorial Centre, ambazo zimeahidi kushirikiana na Tanzania katika utafiti na maendeleo ya teknolojia hiyo.
Wakati huo huo, TAEC ipo katika hatua za awali za kuanzisha mtambo wa kinunurishi (food irradiator) nchini, utakaosaidia kuongeza muda wa uhifadhi wa mazao ya kilimo, kupunguza hasara kwa wakulima na kuboresha usalama wa chakula.
Ushirikiano huo unachukuliwa kuwa wa kimkakati kwa maendeleo ya taifa, ukilenga kuimarisha sekta ya afya, kilimo na utafiti, huku ukichochea matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi.








No comments:
Post a Comment