Na: Jawadu Kinyobwa – Arusha
Serikali imeagiza waajiri na wasimamizi wa rasilimaliwatu nchini kuhakikisha watumishi wote wenye sifa na waliotengewa bajeti ya kupandishwa Vvyeo Mei mwaka huu wanapandishwa vyeo bila kuwapo kwa ucheleweshaji wowote.
Agizo hilo linasisitiza kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kanuni kwa wakati, huku Serikali ikionya kuwa haitavumilia malalamiko ya watumishi ambao haki zao zinakwama kutokana na uzembe wa maafisa utawala.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametoa msimamo huo wakati akifungua mkutano wa pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM Tawi la Tanzania) jijini Arusha Mei 06, 2026.
Amebainisha kuwa Ofisi yake haitegemei kupokea malalamiko ya watumishi walioachwa wenye sifa huku akisisitiza kuwa watumishi waliojiendeleza lazima wabadilishiwe kada kulingana na miongozo iliyowekwa, kwani kufanya kinyume ni kutowajibika ipasavyo.
Waziri Kikwete ameeleza kuwa mageuzi ya utumishi wa umma yanategemea kwa kiasi kikubwa mchango wa wataalamu hao wa utawala na rasilimaliwatu.
Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete ameagiza mabadiliko makubwa ya utendaji kazi ndani ya utumishi wa umma, akisisitiza kuwa kuanzia sasa maafisa rasilimaliwatu na utawala nchini lazima wahakikishe wanajenga usalama wa kisaikolojia kwa watumishi.
Aidha Waziri amebainisha kuwa viongozi hao wana wajibu wa kutengeneza mazingira yanayofikika ili watumishi waweze kueleza changamoto zao bila hofu, hatua itakayosaidia kuepuka msongo wa mawazo na kuimarisha afya ya akili maeneo ya kazi.
Katika msisitizo wa matumizi ya teknolojia, Waziri ameelekeza matumizi kamili ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo e-uhamisho, ambapo amepiga marufuku matumizi ya barua za kawaida katika mchakato wa uhamisho wa watumishi.
Waziri amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia mwongozo wa kujitolea katika utumishi wa umma wa mwaka 2025, akitaka fursa za vijana kutolewa kwa njia ya uwazi na haki bila upendeleo wowote. Aidha, amewataka maafisa hao kuwa viongozi wa mageuzi katika taasisi zao kwa kupunguza urasimu na kushughulikia kero za watumishi katika ngazi ya taasisi badala ya kuziacha kuwa mzigo kwa mamlaka za juu. wananchi.
Vilevile, amewaagiza wataalamu hao kuhakikisha wanazingatia uadilifu na uzalendo kwa kuepuka matumizi ya lugha zisizofaa wanapowahudumia wateja wao, jambo ambalo linaharibu taswira ya serikali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Xavier Daudi, amesema serikali imefanya maboresho ya muundo wa maofisa rasilimali watu tangu Septemba mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kuhuisha mitaala na kuanzisha bodi ya kitaaluma kwa maofisa hao ili kuimarisha maadili na utendaji wao.
Naye Mwenyekiti wa AAPAM tawi la Tanzania, Leila Mavika, amesema zaidi ya washiriki 1,300 wamehudhuria mkutano huo, akibainisha kuwa unatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kiutendaji katika sekta ya rasilimali watu.
Kwa upande wake, Rais wa AAPAM Afrika, Dk,John Nakabago, alisisitiza umuhimu wa serikali kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia kwa wote ili kufanikisha mageuzi ya kidijitali
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment