Thursday, March 19, 2026

UZAZI WA MPANGO: KUVUNJA DHANA POTOFU NA KUIMARISHA NAFASI YA VIJANA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA

 

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
UZAZI wa mpango si mjadala wa kiafya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo ya taifa. Ni nyenzo inayogusa afya ya mama na mtoto, ustawi wa familia, nguvu kazi ya vijana na mustakabali wa uchumi wa nchi. Nchini Tanzania, pamoja na jitihada za serikali na wadau wa maendeleo, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo, dhana potofu na upatikanaji wa huduma hasa kwa vijana.


Kwa mujibu wa tafiti za afya ya uzazi (TDHS), wastani wa mwanamke wa Kitanzania huzaa zaidi ya watoto wanne katika maisha yake ya uzazi. Aidha, chini ya nusu ya wanawake walio kwenye ndoa hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Hii inaashiria pengo la uhitaji wa huduma, hali inayochochea mimba zisizotarajiwa na kuathiri mipango ya familia na taifa kwa ujumla.
Maana na umuhimu wa uzazi wa mpango


Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya afya ya uzazi, jinsia na familia, Dkt Katanta Simwanza, anasema dhana ya uzazi wa mpango ni kupata mtoto kwa kupangilia kutokana na makubaliano ya wenza wote wawili.

Anasema kitaalamu mimba moja hadi nyingine inashauriwa ipishane kwa miaka miwili hadi mitano ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Kwa mujibu wake, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa familia kwani huwapa wazazi muda wa kufanya shughuli za kiuchumi, kuimarisha mahusiano, na kumpa mama nafasi ya kurejesha afya yake baada ya ujauzito.

“Uzazi wa mpango unasaidia mtoto kupata huduma bora, afya njema na kukua katika mazingira mazuri pasipo changamoto,” anasema.
Anabainisha kuwa familia ambazo hazipangi uzazi hukabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uchovu wa kiafya kwa wazazi, watoto kudhoofu kiafya, ukosefu wa elimu na wakati mwingine kunyanyapaliwa katika jamii.

Aidha, anasema mimba zisizo na mpangilio zinaweza kuongeza hatari ya matatizo ya kiafya kwa mama ikiwemo kutoka mimba au kuzaa mtoto mfu.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa ujauzito wa utotoni na mimba za mfululizo huongeza uwezekano wa vifo vya mama na mtoto.

Kwa mujibu wa Dk Simwanza, matumizi ya njia za uzazi wa mpango pia yanaweza kupunguza hatari za kijamii kwa watoto.
“Kwenye jamii zetu kuna watoto wengi ambao ni matokeo ya wazazi kutofuata uzazi wa mpango, baadhi huishia kulelewa mitaani au katika familia nyingine,” anasema.

Anaongeza kuwa bila mpangilio mzuri wa uzazi, familia nyingi hukosa utulivu wa mawasiliano na ushirikiano jambo linaloweza kusababisha changamoto za kiafya, lishe duni na hata vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ushiriki wa wanaume bado mdogo
Licha ya uwekezaji unaofanywa na serikali na wadau katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango, matumizi yake bado yako chini ya asilimia 35.
Dk Simwanza anasema hali hiyo inachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mitazamo ya kidini, dhana potofu na ukosefu wa ushiriki wa wanaume katika maamuzi ya uzazi.

“Uwekezaji mkubwa ulilenga zaidi wanawake wakati mara nyingi wanaume ndio watoa maamuzi katika familia,” anasema.
Anaongeza kuwa wanaume wanapaswa kutambuliwa kama wenza na wateja wa huduma za uzazi wa mpango ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga familia zao.
Vijana na changamoto za kupata taarifa sahihi
Ripoti za kitaifa zinaonyesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya wasichana hupata ujauzito kabla ya kutimiza miaka 18. Mimba za utotoni huchangia utoro wa shule, ndoa za mapema na kuendeleza mzunguko wa umaskini wa kizazi hadi kizazi.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwanafunzi mwa Mwaka wa pili, Rehema Hamidu anasema kikwazo kikubwa kwa vijana ni hofu na aibu wanapohitaji kupata huduma za uzazi wa mpango.

“Tunaogopa kuonekana tumekosea kimaadili hasa tukikutana na wahudumu wa afya wakubwa au tunaowafahamu,” anasema.
Anaongeza kuwa ukosefu wa faragha katika baadhi ya vituo vya afya na utegemezi wa taarifa kutoka mitandao ya kijamii huongeza mkanganyiko kwa vijana.

Kwa upande wake Mark Emmily anasema dhana potofu zimeathiri maamuzi ya vijana wengi, huku baadhi wakiamini kuwa uzazi wa mpango husababisha ugumba au saratani.
Hata hivyo, Dkt Simwanza anasisitiza kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango husababisha ugumba wa kudumu.
Mtazamo wa dini katika uzazi wa mpango
Katika jamii ambayo dini ina ushawishi mkubwa katika maamuzi ya familia, viongozi wa dini pia wanaona umuhimu wa kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi.

Mchungaji na mdau wa maendeleo James Mlali anasema dini nyingi zinakubaliana kuhusu umuhimu wa kupishanisha watoto kwa muda unaofaa ili kulinda afya ya mama na mtoto.

“Dini zote zinahimiza kutoa nafasi kati ya mtoto na mtoto angalau miaka miwili, ambayo pia ni kipindi cha msingi cha unyonyeshaji wa mtoto,” anasema.

Kwa mujibu wake, mafundisho ya dini yanaweka msingi wa uwajibikaji katika malezi ya familia.

Anasema katika Biblia Takatifu kuna mafundisho yanayohimiza watu kuwajibika kwa familia zao na kuhakikisha wanawapatia watoto mahitaji muhimu.

Anaongeza kuwa hata katika Qur'an mafundisho yanasisitiza umuhimu wa kuwahudumia wake na watoto kwa haki na uwezo.

Mlali anaona taasisi za dini zina nafasi kubwa katika kuwapa vijana elimu sahihi kuhusu masuala ya familia, afya ya uzazi na maadili.

“Ni muhimu vijana wakapewa elimu sahihi wawapo misikitini na makanisani ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao ya baadaye,” anasema.

Anasisitiza kuwa mila za kitamaduni kama jando na unyago zinaweza pia kuboreshwa ili kujumuisha elimu ya afya ya uzazi na kuwasaidia vijana kuelewa masuala ya familia kwa kina.

"Uzazi wa mpango ni kitu muhimu sana kwa vijana kwani vijana ambao hawana majukumu ya kifamilia huduma za afya ha uzazi ni nzuri katika kuamua wakati wa kuzaa, kupishanisha kwa muda gani na mara ngapi wabebe mimba hiyo muhimu kwa afya zao na kuweka mipango ya maendeleo," anasema.

Mchungaji Mlali anasema kupanga uzazi ni muhimu katika kuwapatia watoto huduma za lishe, elimu na masuala ya kisaikolojia.

Anasisitiza kwamba kuna makanisa yanaunga mkono njia za uzazi wa mpango wa asili na kisasa na Kanisa Katoliki linahimiza njia za asili pekee kulingana na mahitaji yao na afya ya wanaohitaji huduma hizo.

Hatua za serikali na wadau
Serikali imeendelea kuimarisha sera na mipango ya kuboresha huduma za uzazi wa mpango kupitia Wizara ya Afya pamoja na ushirikiano wa wadau wa maendeleo.

Hatua hizo zinahusisha kuandaa wataalamu wa kutoa huduma za uzazi wa mpango wa muda mfupi na mrefu, pamoja na kusambaza elimu katika maeneo ya vijijini kupitia huduma za mkoba.

Aidha, katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uzazi wa mpango umepewa kipaumbele kama sehemu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, mimba zisizotarajiwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kwa ujumla, uzazi wa mpango ni zaidi ya suala la afya ni mkakati wa kijamii na kiuchumi unaogusa maendeleo ya taifa. Ushirikiano kati ya serikali, wataalamu wa afya, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla unaweza kusaidia kuvunja dhana potofu na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi.

Kuwapa vijana taarifa sahihi, huduma rafiki na mazingira salama ya kuuliza maswali ni hatua muhimu katika kulinda mustakabali wa taifa. Tanzania yenye vijana wenye taarifa sahihi na maamuzi bora ndiyo Tanzania yenye maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment