Tuesday, March 24, 2026

NEMC YAHAMASISHA UBUNIFU WA BIDHAA ZITOKANAZO NA TAKA

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na wadau wa mazingira, linatarajia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Taka “Taka Sifuri” kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kubadilisha taka kuwa malighafi au bidhaa nyingine, hatua inayolenga kuifanya taka kuwa fursa ya kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 24, 2026, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamadi Kissiwa, amesema maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia Machi 28 hadi Machi 30, 2026 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Amesema kaulimbiu ya kimataifa ya maadhimisho hayo ni “Wezesha taka sifuri kwenye sekta ya chakula”, huku kaulimbiu ya kitaifa ikiwa ni “Taka ni Fursa”. Ameongeza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.

Kissiwa amefafanua kuwa lengo kuu la maadhimisho hayo ni kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu taka, kwa kuhamasisha matumizi ya dhana ya 3Rs ambayo ni Kupunguza (Reduce), Kutumia tena (Reuse) na Kurejeleza (Recycle), ili kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali na kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Amesema matumizi ya mbinu hizo yatasaidia kupunguza kiwango cha taka kinachotupwa ovyo, huku yakichangia upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa nyingine, hali itakayosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Aidha, ameeleza kuwa maadhimisho hayo pia yanalenga kuangazia changamoto ya upotevu wa chakula duniani, ambapo takwimu zinaonesha kuwa utupaji wa chakula unachangia takribani asilimia 10 ya uzalishaji wa hewa chafuzi, hali inayochangia mabadiliko ya tabianchi na kuathiri ustawi wa jamii.

Mbali na hilo, Kissiwa amewakaribisha wananchi na wadau wa mazingira kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 11 jioni, yakijumuisha maonesho ya fursa za uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa taka pamoja na ubunifu wa bidhaa zitokanazo na taka.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya “taka sifuri”, ambayo inalenga kujenga jamii inayotambua thamani ya taka na kuzitumia kama rasilimali badala ya kuziona kama uchafu.







No comments:

Post a Comment