WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara nchini kutowaumiza Watanzania kwa kupandisha bei za bidhaa hususani kipindi hiki cha kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na mfungo wa Kwaresma kwa kuwa nchi kwa sasa haina upungufu wa chakula.Amesema licha ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) nchini kutangaza kuwepo kwa upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini lakini nchi inautoshelevu wa chakula hivyo hakuna sababu ya kupandisha bei za vyakula.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Januari 29, wakati akijibu swali la Nancy Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali imejipangaje kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula na kuzuia mfumuko wa bei kuelekea kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma.
“…Kwa sasa tunachakula cha kutosha, mahitaji ya chakula cha akiba kwa nchi ni takribani tani 150,000 na sasa nchi ina zaidi ya tani 400,000 za akiba ya chakula rai ambayo niliitoa hata nilipokutana na wakuu wa mikoa ni kuendelea kuwahamasisha wananchi kuzingatia ushauri wa aina ya mazao ya kupanda.”
Pia, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini wawaelimishe wananchi kuendelea kutumia vizuri chakula walichonacho kutokana na tahadhari ya upungufu wa mvua iliyotolewa na TMA. “Wananchi watunze chakula na kuwa na matumizi ya lazima tu, ili kuweza kuwa na akiba.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Afya kuzingatia viwango rasmi vya gharama za huduma na kuharakisha mpango wa kutunga sheria itakayoweka viwango vinavyofanana nchini kote, ili kuondoa hali ya baadhi ya maeneo kuwa na viwango tofauti.
Ametoa maelekezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani ambaye alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu viwango wanavyotozwa wananchi kama gharama ya kumuona daktari ambaye ni mwajiriwa na analipwa mshahara na Serikali.
Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa utaratibu wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, wananchi wanahimizwa kujiunga na mifumo ya bima ili kupunguza changamoto ya kuchangia gharama wanapohitaji huduma hospitalini.
Waziri Mkuu amefafanua kuwa makundi yaliyoainishwa kisheria kama watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wazee na wenye magonjwa ya mlipuko yanaendelea kupata msamaha wa kuchangia gharama hizo.
Kuhusu changamoto ya mifumo hospitalini, Waziri Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa karibu ili kuondoa uzembe na visingizio vinavyochelewesha wagonjwa, huku taasisi husika zikielekezwa kurekebisha mapungufu ya kimfumo kwa kuwa huduma za afya hazipaswi kusubiri.

.jpeg)
No comments:
Post a Comment