HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 8, 2024

SERIKALI YAWAPONGEZA WAGANI KWA KUSAIDIA NCHI KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA

 

 

Na: Calvin Gwabara - Dodoma.



Serikali yakipongeza Chama cha Maafisa ugani Tanzania (TSAEE) kwa kazi nzuri inayofanywa na wagani hao nchi nzima katika kusaidia wakulima,wafugaji na wavuvi kuzalisha kwa tija na kupelekea nchi kujitosheleza kwa chakula hasa nafaka.

Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mratibu wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Bw. Wilson Shimo wakati akifunga Kongamano la maafisa ugani nchini lililoandaliwa na (TSAEE) na kuwakutanisha wagani katika sekta ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi kutoka nchi nzima ili kujifunza teknolojia mbalimbali mpya zinazooneshwa mwaka huu kwenye maonesho ya Kilimo Nanenane kitaifa.

“Nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa niaba ya Serikali kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya ya kutumia utaalamu wenu kutoa ushauri wa kitaalamu kwa jamii kwenye sekta zote tatu za Kilimo,Mifugo na Uvuvi kuweza kuongeza tija na kupelekea utoshelevu wa chakula katika nchi yetu hususani katika Kilimo cha nafaka na ndio maana serikali inaendelea kuboresha mazingira yenu ya kazi ili mfanye kazi vizuri zaidi”alisema Bw. Shimo.

Aliongeza “Kwa kutambua mchango wenu na kuboresha mazingira yenu ya utoaji huduma Serikali imenunua magari 15, Pikipiki kwa maafisa ugani nchi nzima, Vishikwambi 4305, Vifaa vya kupima udongo na ujenzi wa nyumba 50 za maafisa ugani kwenye ngazi za kata unaendelea, hii ni sehemu tu ya mengi ambayo Serikali inayafanya katika kuboresha utendaji wenu na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuchochea ufanisi hivyo juhudi hizo za serikali ziwafanye muendelee kuwajibika kwenye maeneo yenu”.

Amesema jukumu la kuwapatia maafisa ugani mafunzo rejea sambamba na vitendea kazi ni la wizara zote za Kisekta kwa kushirikiana na ofisi ya Rais TAMISEMI hivyo ni muhimu kuendelea kukumbushana katika umoja huo na kupitia kwa Chama chao ili wataalamu hao ili kupunguza changamoto zinazowakabili kama sio kuzimaliza kabisa.

Amesema hadi sasa Tanzania kuna maafisa kilimo ugani 7000 kwa upande wa kilimo, Mifugo wapo 3642 na Uvuvi wapo 647 na kwa takwimu hizo inaonesha kuwa idadi hiyo bado ni ndogo ikilinganishwa na maeneo yaliyopo kwani zipo kata 3659,vijiji 12,319,Mitaa 4,233 na haya yote yanahitaji kuwa na wagani lakini pamoja na uchache wao lakini wanatoa huduma nzuri kukidhi mahitaji.
Nae kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) Prof. Catherine Msuya kutoka Chuo Kikuu ch Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema chama hicho kimeanzishwa mahususi kwa lengo la kuwakutanisha wagani kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kubuni mbinu za pamoja za kusaidia utoaji wao wa huduma kwa jamii ili kusaidia kuongeza tija na kuinua uchumi wa Taifa.

“Tunafarijika sana kama chama kuona serikali inatambua mchango wetu kama maafisa ugani katika kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula kwa kipindi kirefu,pia tunamshukuru sana Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wagani na kuboresha mazingira yao ya kazi katika kutoa huduma kwa kuwanunulia wagani Pikipiki nchi nzima na vifaa vingine ikiwemo vya kupima udongo na mengine mengi anayoyafanya kwakweli anatutia moyo sana na kuongeza ari ya wagani katika kutoa huduma bora zaidi” alieleza Mwenyekiti wa TSAEE Prof. Catherine .

Amesema mwaka huu wamekutana kwenye kongamano la Chama chao wakati wa Maonesho ya Nanenane Jijini Dodoma ili kujifunza teknolojia na mbinu mbalimbali zinazooneshwa kwenye maonesho hayo ya kitaifa na kujadiliana namna ya kuzipeleka kwa wakulima kwenye maeneo wanayotoka na kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe alilolitoa mwaka jana kwenye mkuatano wao wa mwaka.

Prof. Catherine amesema Chama hicho kitaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo maafisa ugani hao kwenye utoaji wa huduma kwa jamii ikiwemo mafunzo rejea ili waweze kupata taarifa mpya na tenkolojia mbalimbali za kisasa zinazozalishwa.

TSAEE imewakutanisha maafisa ugani kutoka nchi nzima kwenye maonesho hayo ya Nanenane kitaifa yanayofanyika Jijini Dodoma kwenye Kongamano la siku tatu na kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazooneshwa mwaka huu pamoja na kupata uzoefu kutoka kwa wataalamu kutoka Marekani na China walioshiriki kongamano hilo.
Mratibu wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Bw. Wilson Shimo wakati akifunga Kongamano la maafisa ugani nchini lililoandaliwa na (TSAEE).

Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) Prof. Catherine Msuya na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akieleza malengo ya Kongamano hilo.

Prof. Dismas Mwaseba kutoa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA akitoa uzoefu wake na mchango wake kwenye kongamano hilo.

Prof. Carol Smathers kutoka Chuo Kikuu cha Ohio nchini Marekani ambaye ni mdau wa TSAEE akieleza uzoefu wake wa matumizi ya Ugani kwenye kuwezesha kilimo na nafasi Umuhimu wa Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kujifunza kilimo.






Maafisa Ugani wakifuatilia hotuba ya ufungaji wa kongamano hilo la siku tatu Jijini Dodoma.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad