HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 14, 2023

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YATEMBELEA NIMR, YAACHA MAAGIZO

 Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud wa akimkabidhi zawadi Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Afya na Masuala ya Ukimwi Stansalus Nyongo wakati wa ziara ya wabunge hao katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) anayeshudia hi Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Faustine Ndungulile. Ziara hiyo imefanyika  leo Septemba 14, Mabibo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud aliyesimama  akizungumza na wabunge pamoja na wadau mbali mbali wa afya wakati wa ziara ya wabunge hao katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) iliyofanyika leo Septemba 14, Mabibo jijini Dar es SalaamMkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud akizungumza na wabunge pamoja na wadau mbali mbali wa afya wakati wa ziara ya wabunge hao katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) iliyofanyika leo Septemba 14, Mabibo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi,  Stanslaus Nyongo (katikati)  akizungumza na wabunge pamoja na wadau mbali mbali wa afya wakati wa ziara ya wabunge hao katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) iliyofanyika leo Septemba 14, Mabibo jijini Dar es Salaam.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi, imeelekeza Wizara ya Afya na Baraza la Tiba za asili kuhakikisha wanaweka mkazo katika sheria ya tiba asili ili mtu anayeuza dawa hizo ziwe na ubora na usalama kwa mtumiaji.

Akizungumza Leo Dar es Salaam katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo amesema lengo la ziara hiyo ni kutembelea kitengo cha utafiti wa tiba asili kwani Tanzania ina miti mingi na serikali ina jukumu la kuhakikisha tiba asili inachukua nafasi yake.

Amesema kuwa kwa kiasi kikubwa wameridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali katika kuona usalama wa dawa za asili ili Watanzania watumie wakiwa na uhakika kuwa dawa hizo ni salama.

"Ni muhimu kujua usalama wa dawa za asili ili kuepusha Watanzania kununua dawa bila kujua kama dawa husika ni salama na haina viambata vya sumu na wakati mwingine zipo feki na huharibu figo na viungo vingine vya mwili," amesema Nyongo.

Ameeleza kuwa ni muhimu kufanyika utafiti kwa dawa za asili ili kujua usalama wake na matumizi salama ya dawa hizo.

"Hapa kuna kama kiwanda ambacho serikali hukusanya dawa kutoka maeneo mbalimbali na kuna wadau mmoja mmoja ambao huleta dawa zao ili kufanyiwa utafiti hivyo pia inawezesha uzalishaji wa dawa za asili kwa ajili ya matumizi salama ya binadamu," amesema.

Amefafanua kuwa jukumu lao ni kuishauri serikali hususan kutenga bajeti kuhakikisha juhudi hizo zinafanikiwa na mipango iliyopangwa inatekelezeka.

Pia amesema baraza la tiba asilia linapaswa kuhakikisha dawa zote zinazotumika zimekidhi vigezo ili kuondoa watu wasio na wanaouza dawa mtaani kwa kile wanachodai hutibu magonjwa mbalimbali.

"Tumeambiwa na wataalamu wapo watu ambao wanauza dawa za asili ambazo wanadai zinatibu nguvu za kiume kumbe ndani yake zimewekwa Viagra hivyo mtu akitumia vibaya zinaweza kumsababishia madhara,"

Nyongo amesema: "Tunataka kama dawa ya asili inayouzwa inatibu ugonjwa fulani kama vile ugonjwa wa moyo, sukari na nguvu za kiume basi iwe kweli na chombo hiki ndio kinatakiwa kuhakikisha ubora huo kabla ya kusajili dawa," ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NIMR, Profesa Said Aboud amesema wana jukumu lakufanya utafiti kuangalia usalama, usahihi na ubora wa dawa zote ikiwemo za asili.

Amesema suala la utafiti kuchukua muda mrefu ni jambo la kawaida kutegemea na aina ya utafiti unaofanyika kwani kama unahusu magonjwa ya binadamu ni lazima wapitie hatua mbalimbali ili kupata matokeo na ni hatari kuharakisha.

Kuhusu tozo, Profesa Aboud amesema wanapata fedha kutoka serikalini kwa ajili ya utafiti na kutokana na maelekezo yaliyotolewa wataangalia namna bora ya kutoza watu ada wanaotaka kufanyiwa tafiti zao.

Amesema baraza la tiba asili kuna ada ambayo inawatoza watu wenye kliniki za tiba asili na wanaotoa tiba asili wakitaka kusajiliwa.

Amesema kuwa waganga wa tiba asili kupitia vyama vyao 28, wanahamasishwa kushirikisha NIMR kufanya tafiti kwenye dawa zao za tiba asili wanazogundua na kwamba hakuna watu watakaowanyang'anya.

Amesema lengo la kufanya utafiti ni kuangalia ubora, ufanisi na usalama wa dawa hizo ili mtumiaji asipate madhara pale ambapo ataitumia.

"Tunaendelea kuhamasisha wadau wa tiba asili kuona umuhimu wa kuleta dawa wanazogundua ili tuzifanyie utafiti na mwisho wa siku tuone ubora na usalama wao," amesema.

Kuhusu utafiti wa Ukimwi, Mkurugenzi huyo amesema Kituo cha NIMR Mbeya inashiriki katika utafiti unaohusisha nchi tatu za Afrika kupitia taasisi nne.

Amesema katika utafiti huo, unajumuisha utolewaji wa chanjo na dawa kinga na kwamba utafiti huo ni wa awamu ya pili.

"Utafiti huu unashirikisha washiriki waliokwenye hatari ya kupata maambukizi ya Ukimwi hivyo tunaangalia kama chanjo na dawa kinga hizi zitaweza kumkinga kupata maambukizi mapya. Utafiti huu ulianza mwaka 2018 na unatagemea kuhitimishwa Juni 2024 na watatoa matokeo," amesisitiza Profesa Aboud.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad