UBIA kati ya Marekani na Tanzania umekita mizizi katika zaidi ya miongo sita ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, maendeleo, afya na usalama. Marekani na Tanzania zinasimama pamoja kama marafiki na wabia, kwa kuzingatia misingi ya kuheshimiana na malengo ya pamoja ya kuwa na mustakabali wenye amani na ustawi zaidi. Marekani inaunga mkono kikamilifu ajenda ya Tanzania ya mageuzi ya kidemokrasia na ina dhamira thabiti ya kusaidia kuendeleza maadili ya kidemokrasia ya Tanzania. Ziara ya Makamu wa Rais nchini Tanzania inathibitisha ubia huu imara baina ya nchi zetu mbili na itaimarisha zaidi ushirikiano katika biashara, jitihada za kutafuta ufumbuzi kuhusu usalama na uhakika wa chakula, ulinzi wa bayoanuai za majini, uwekezaji kwa wanawake na vijana, afya na kuimarisha demokrasia. Katika kusaidia kuongeza wigo na kina cha uhusiano wetu rasmi, Serikali ya Marekani inakusudia kutoa Dola za Kimarekani milioni 560 kama msaada rasmi kwa Tanzania katika mwaka wa fedha wa 2024. Kama sehemu ya ziara yake Dar es Salaam, Makamu wa Rais anatanga ahadi zifuatazo za Marekani kwa Tanzania: Kuimarisha Mahusiano ya Kibiashara
• Kuzinduliwa kwa Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania: Tarehe 31 Machi, Wizara ya Biashara na Viwanda ya Tanzania na Wizara ya Biashara ya Marekani zinatarajia kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) kuanzisha majadiliano rasmi ya kibiashara baina ya nchi zetu mbili. Majadiliano hayo yataanzisha vikosi kazi (working groups) vikiwa na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani na Serikali ya Tanzania, vikifuatiwa na mkutano wa mwaka wa wakuu wa taasisi (principals), kujadili jinsi ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na Tanzania. Majadiliano hayo yatalenga katika maeneo makuu manne: uchumi wa kidijitali; namna ya kuyafikia masoko ya Marekani; mabadiliko ya kanuni na mazingira ya kufanyia biashara; na ziara za kibiashara (trade missions). Majadiliano haya yatashughulikia moja kwa moja vikwazo vinavyokwamisha kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kwa lengo la kupanua maeneo lengwa haya manne ya mwanzo katika kipindi cha miaka mitatu ya makubaliano haya.
• Hati ya Makubaliano (MOU) kati ya Benki ya EXIM ya Marekani na Tanzania: Hati ya Makubaliano itakayosainiwa kati ya Benki ya EXIM ya Marekani na Serikali ya Tanzania itapanua ushirikiano wa kibiashara baina ya Marekani na Tanzania kwa kuziwezesha kampuni za Kimarekani kuleta (export) nchini Tanzania bidhaa na huduma bora za kibunifu. Hati hii ya Makubaliano ambayo itawezesha upatikanaji wa hadi Dola za Kimarekani milioni 500 kugharimia upelekaji wa huduma na bidhaa (export financing) Tanzania, itasaidia upelekaji wa bidhaa na huduma hizo katika sekta mbalimbali hususan, miundombinu, usafirishaji, teknolojia ya kidijitali, nishati na miradi ya nishati jadidifu. Kwa kuimarisha na kuongeza fursa za kiuchumi, makubaliano haya yatasaidia kukuza ajira nchini Tanzania na Marekani. Aidha, makubaliano haya yanathibitisha azima ya dhati ya Serikali ya Marekani ya kuhuisha ubia na ushirikiano na Afrika na kujenga dhima rasmi ambayo EXIM imepewa na Bunge la Marekani ya kuongeza na kuimarisha uhusiano kati ya wafanyabiashara wa Kimarekani wanaouza bidhaa na huduma nje ya Marekani (exporters) na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.]
• Huduma za Ushari kuhusu Uendeshaji na Biashara ya Bandari (Port Transaction Advisory Services): Marekani inatoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa Serikali ya Tanzania. Programu ya Tanzania ya Huduma ya Ushauri kuhusu Uendeshaji na Biashara ya Bandari inalenga kusaidia jitihada za Serikali ya Tanzania kutumia kikamilifu fursa za uwekezaji na kuvutia wawekezaji wa aina mbalimbali, kulinda uwekezaji wake wa kifedha na kuimarisha udhibiti wake, kama nchi huru, wa miundombinu hii muhimu.
• Kuletwa kwa Ndege ya Boeing: Boeing imetangaza kuwa tarehe 31 Machi itakabidhi moja kati ya ndege nne zitakazoongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya ndege za Shirika la Ndege la Tanzania. Kukabidhiwa kwa ndege ya mizigo ya 767-freighter kutaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara ya usafirishaji mizigo, ikiwawezesha wazalishaji wa Kitanzania na wa Afrika Mashariki kuyafikia masoko ya kimataifa kwa haraka na ufanisi. Ndege nyingine tatu za abiria, moja aina ya 787 Dreamliner, na mbili aina ya 737-MAX, zitafungua masoko mapya ya usafiri na sekta ya utalii nchini Tanzania, hivyo kuongeza nafasi za ajira. Ndege pamoja na teknolojia ya usafiri wa anga zilizohusika katika mauziano haya zimezalisha maelfu ya nafasi za ajira nchini Marekani na zitaboresha uwezo wa ushindani wa kiuchumi wa Tanzania.
• Mradi wa Life Zone Metals: Marekani kupitia Mpango wa Ubia kwa Uwekezaji wa Kimataifa katika Miundombinu (Partnership for Global Infrastructure Investment - PGII), ambao ni mradi wa serikali ya Marekani kuwezesha kuendelezwa kwa miundombinu yenye kuleta maendeleo, umesaidia kuanzishwa kwa ubia wa kimkakati kati ya Life Zone Metals na TechMet; makampuni yanayoongoza katika uzalishaji wa metali muhimu ambayo kwa sehemu yanamilikiwa na Serikali ya Marekani kupitia DFC. Life Zone Metals imeingia makubaliano (Framework Agreement) na Serikali ya Tanzania kufungua kiwanda cha kuchakata/kuchenjua aina mbalimbali za metali kwa kutumia teknolojia ya kisasa isiyochafua mazingira. Kiwanda hicho kichenjua madini ya nickel na madini mengine muhimu yanayochimbwa Tanzania, kikilenga kuzalisha nickel iliyotayari kutengenezea betri kwa ajili ya kupelekwa Marekani na soko la kimataifa ifikapo mwaka 2026. Ubia huu utafanya kazi ya kutafuta fursa za ziada katika kanda kwa ajili ya kupata madini mengine muhimu ya kuchenjua katika kiwanda hicho kipya. Life Zone Metals itaanzisha kiwanda hicho mahali ambapo palikuwa na mgodi wa zamani wa dhahabu wa Barrick. Tunaunga mkono ubia wa aina hii katika uzalishaji na tunapongeza uwepo wa kampuni ya Barrick nchini, ikiwa ni pamoja na ahadi yake ya hivi karibuni ya kutenga Dola za Kimarekani milioni 30 kwa ajili ya kujenga shule 160 nchini kote Tanzania. Jitihada hizi zinalenga kujenga na kupanua mnyororo wa ugavi kwa teknolojia ya nishati safi ulio imara na wenye uwazi, uliojengwa katika misingi ya kuwashirikisha kikamilifu wenyeji, unaoheshimu na kuzingatia mazingira na uhifadhi, usalama, na kanuni za kazi zinazozingatia utu na maadili.
• Mkongo wa Mawasiliano unaotumia Fiber (Fiber Backbone) na Kupanua Mtandao wa Intaneti katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati: Idara ya Biashara na Maendeleo ya Marekani (U.S. Trade and Development Agency - USTDA) itasaidia kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya intaneti kwa gharama nafuu kwa maelfu ya watu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kupitia ruzuku ya Dola za Kimarekani milioni 1 kwa ajili ya kufanya utafiti na upembuzi yakinifu kusaidia kuanzishwa kwa mkongo mpya wa mawasilino (fiber backbone) na kujenga miundombinu kuwezesha upatikanaji wa huduma za kimtandao katika nchi za Tanzania, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
• Uwekezaji wa Kampuni ya Irvine katika Biashara ya Ufugaji Kuku: Tarehe 30 Machi, Kampuni ya Irvine, inayojihusisha na biashara ya ufugaji kuku katika nchi mbalimbali barani Afrika, ambayo inamilikiwa kwa pamoja na wawakezaji wa Kimarekani, ilitangaza uwekezaji wa ziada wa Dola za Kimarekani milioni 31 katika sekta ya ufugaji kuku nchini Tanzania. Uwekezaji huu utawezesha kuhakikishwa kwa usalama wa chakula, kuongeza upatikanaji wa uhakika wa kuku (protini) bora katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na kutengeneza fursa ya kipato kwa maelfu ya wafugaji wa Kitanzania, wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana. Tanzania itanufaika kutokana na uwekezaji huu kwa kuwa utapanua uzalishaji wa vifaranga pamoja na kuanzisha kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo. Shughuli hizi zitakazofanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa zitahitaji wafanyakazi wenye ujuzi na stadi kubwa ikiwa ni pamoja na wanasayansi wa mifugo, wataalamu wa lishe, madaktari wa mifugo, wataalamu wa maabara na wafanyakazi wa kada nyingine za kitaalamu.
● Ubia Katika Teknolojia ya Mawasiliano ya 5G na Usalama Mtandaoni: Wakati wa mkutano wao wa Aprili 2022, Rais Samia na Makamu wa Rais Harris waliahidi kujielekeza katika kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania katika maeneo ya usalama wa mtandao (cybersecurity) na teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA). Toka wakati huo, Marekani imefanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania kuendesha warsha ya kikanda kuhusu TEHAMA; imetoa msaada wa kitaalamu kuhusu teknolojia ya 5G, usalama wa mtandao, na kupambana na uhalifu mtandaoni, pamoja na kuwezesha uwekezaji mkubwa zaidi wa wawekezaji wa Kimarekani katika sekta ya TEHAMA nchini Tanzania. Tarehe 23 Machi, Marekani na Tanzania zilisaini hati ya makubaliano kuanzisha ubia wa kimkakati wa kujenga uwezo na kushirikiana katika teknolojia ya 5G, usalama wa mtandao na sera, kanuni na sheria zinazohusiana na mambo hayo. Kuwekeza katika Demokrasia, Utawala Bora na Maendeleo
• Ushirikiano Rasmi kati ya Marekani na Tanzania katika Maendeleo: Tarehe 29 Machi, Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) na Serikali ya Tanzania zilisaini makubaliano ya miaka mitano ya msaada wenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani bilioni 1.1. Chini ya makubaliano hayo, USAID itafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania kutoa msaada katika maeneo ya ukuaji uchumi, afya, elimu, demokrasia na utawala bora. Makubalino haya yanathibitisha dhamira ya dhati ya serikali ya Marekani kusaidia kuendeleza vipaumbele vya maendeleo vya Seikali ya Tanzania.
• Kuimarisha Haki za Kidemokrasia na Utawala Bora: Katika maombi yake ya bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024, utawala wa Biden-Harris umetenga takriban Dola za Kimarekani milioni 16.4 kugharimia programu zinazohusu demokrasia, haki na utawala nchini Tanzania. Hili ni ongezeko kubwa la msaada kwa jitihada za Tanzania katika eneo hili. Zaidi ya hayo, USAID imeichagua Tanzania kama nchi itakayopokea usaidizi kusaidia jitihada zake za kukuza ushiriki wa wanawake na wasichana katika uongozi wa kiraia na kisiasa, hivyo kutoa takriban Dola za Kimarekani Milioni 1 za ziada kugharimia programu hizi kuanzia mwaka huu.
• Kukuza Uhuru wa Kujieleza nchini Tanzania: Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inapanga kutoa Dola za Kimarekani milioni 1 kwa ajili ya miradi itakayohimiza kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza wa umma wa Kitanzania na vyombo vya habari.
• Programu za Kituo cha Demokrasia Tanzania: Katika kusaidia azma ya Tanzania ya kuimarisha demokrasia, hususan nchi inapoelekea katika chaguzi za mwaka 2024 na 2025, Marekani itatoa Dola 400,000 kusaidia Kituo cha Demokrasia Tanzania kuwaleta pamoja wadau kujadili zaidi mageuzi ya kidemokrasia na kisheria, wakati huo huo kikijenga uwezo wa vijana kushiriki katika siasa. Kuimarisha Bioanuai na Usalama wa Chakula.
• Programu ya Heshimu Bahari: Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) linatarajia kutoa Dola za Kimarekani milioni 8.4 kuzindua programu ya Heshimu Bahari, programu ya miaka mitano ya kuimarisha uthabiti wa kiikolojia (ecological resilience) na tija ya mfumo wa ikolojia ya bahari wa Tanzania. Ufadhili huu utaifanya programu ya Heshimu Bahari kuwa mradi kinara katika uwekezaji wa USAID/Tanzania wa Dola za Kimarekani milioni 25 katika jitihada za uhifadhi wa bahari na kusaidia uvuvi endelevu. Tanzania ni kitovu cha bioanuai ya baharini duniani inayowawezesha watu kujikimu kupitia shughuli za uvuvi na utalii, shughuli ambazo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii za pwani visiwani kote Zanzibar na Tanzania bara.
• Kuzinduliwa kwa Mradi wa Kilimo Tija: USAID inatarajia kutoa Dola za Kimarekani milioni 16 kuzindua mradi wa Kilimo Tija, mradi wa kuwasadia wakulima wa Kitanzania, ukiwalenga wanawake na vijana na ukitoa suluhisho la janga la upungufu wa chakula duniani. Mradi wa Kilimo Tija utawapatia wakulima wa Kitanzania pembejeo, rasilimali na utaalamu unaohitajika ili kuongeza mavuno na kuimarisha mnyororo wa ugavi katika uzalishaji wa mbogamboga na matunda ili kuwawezesha wakulima kufikisha mazao yao katika masoko ya ndani na ya kimataifa. Kupitia mbegu bora zinazohimili mabadiliko ya hali ya tabianchi (climate smart seeds) na teknolojia mpya, uwekezaji huu wa serikali ya Marekani utasaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi wakati huohuo ukiongeza uzalishaji wa mazao yenye virutubisho vingi. USAID itatoa Dola za Kimarekani milioni 10 nyingine kama fungu la ziada kwa Ukraine kusaidia hatua za kukabiliana na mzozo wa chakula duniani. Kukuza Elimu, Ushiriki wa Vijana na Kuwajengea Wanawake Uwezo wa Kiuchumi
• Kongamano la Wajasiriamali Wanawake: Takriban wahitimu 100 wa Programu ya Mafunzo kwa Wajasiriamali Wanawake (AWE) kutoka nchi kadhaa za Afrika watakutana nchini Tanzania mwezi Julai kuchangia mbinu bora za kukuza biashara, kukuza uwezo wao wa kupeleka bidhaa zao nje ya nchi zao, kukuza sera jumuishi za kijinsia, na kujenga mtandao imara wa kimataifa wa wanawake katika biashara. Hili litakuwa kongamano la kwanza la wahitimu wa AWE barani Afrika na litahudhuriwa na watoa mada mbalimbali, ikiwemo Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman, kujadili ujasiriamali, upatikanaji wa mitaji, memejimenti ya biashara na fedha na masoko.
• Kongamano la Wahitimu wa Programu ya Humphrey kuhusu Usalama wa Chakula: Mwezi Aprili 2023, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani itawakutanisha jijini Dar es Salaam wahitimu wa Programu ya Humphrey Fellowship, ambayo ni sehemu ya programu wa mabadilishano ya kielimu ya Fulbright Exchange, katika kongamano litakalolenga kupata ufumbuzi (solutions-focused) katika kukuza usalama wa chakula na kuweka mifumo thabiti ya uhakika wa chakula barani Afrika. Wakirejea katika matokeo ya Mkutano wa Kilele wa Viongozi wa Marekani na Afrika, wahitimu hawa wataongoza majadiliano ya kina kuhusu usimamizi endelevu wa ardhi na maji, teknolojia za kilimo na masuala yanayohusiana na hayo. Kongamano hili litaonyesha mchango na umuhimu wa Wahitimu wa Programu ya Humphrey kutoka nchi mbalimbali za Afrika katika kutatua changamoto ngumu za kikanda na kimataifa. Kukuza Ushirikiano katika Sekta ya Afya
Kushirikiana katika kupambana na Marburg: Serikali ya Marekani inashirikiana na Serikali ya Tanzania na wabia katika ngazi zote kusaidia jitihada za Tanzania za kukabiliana na mlipuko wa hivi karibuni wa virusi vya Marburg. Tukutumia ushirikiano wetu wa muda mrefu katika sekta ya afya, Serikali ya Marekani kupitia Kituo cha Marekani cha Udhibiti wa Maradhi (CDC) inatoa msaada wa kitaalamu katika udhibiti wa janga hili. Zaidi ya hayo, USAID inapanga kutoa Dola za Kimarekani milioni 1.3 kwa shughuli za kinga na shughuli nyingine za kimatibabu zitakazosimamiwa wa WHO na UNICEF. Aidha, Marekani inatoa vifaa na mavazi ya kujikinga (Personal Protective Equipment) kuwasaidia wahudumu wa afya wa Kitanzania wanaopambana na mlipuko huu.
• Kuendelea na Uwekezaji wa PEPFAR: Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) mwaka huu ulisherehekea miaka 20 toka kuanzishwa kwake. Kwa kutambua hatua kubwa iliyopigwa na programu ya PEPFAR nchini Tanzania, Serikali ya Marekani inapanga kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 433 katika kipindi cha miaka miwili ijayo na imeomba fedha za ziada kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 395 kwa ajili ya Bajeti ya Rais kwa Mwaka wa Fedha 2024, hii ikitegemea kuidhinishwa kwa fedha hizo na Bunge la Marekani. Tanzania ni mojawapo ya nchi 12 zinazoshiriki katika Muungano wa Kimataifa Kutokomeza UKIMWI kwa Watoto, muungano unaoongozwa na Shirika ya UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) na Ofisi ya Mratibu wa Shughuli za Kupambana na UKIMWI Kimataifa. Kwa ubia na Serikali ya Tanzania, PEPFAR inasaidia kuandaliwa kwa sera za afya zitakazoimarisha programu na afua za VVU kwa watoto. Aidha, PEPFAR inaisaidia Tanzania kuweka sera za afya zitakazoimarisha afua dhidi ya VVU zinazowalenga Watoto. Aidha, PEPFAR inaisaidia Tanzania kupanua shughuli za kinga kwa wasichana na wanawake vijana ambao ndio kundi linaloambukizwa kwa wingi na kasi kubwa zaidi nchini Tanzania.
• Uwekezaji dhidi ya Malaria kupitia Mpango Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI): Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) unapanga kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 39 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao katika ubi ana Serikali ya Tanzania katika kuendesha miradi ya kupambana na malaria iliyothibitika kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na vyandarua, dawa dhidi ya malaria zinazofanya kazi kwa haraka, vifaa vya upimaji wa haraka, na matibabu kinga kwa akina mama wajawazito. Fedha hizi zinakusudiwa kusaidia mfumo ulioimarishwa zaidi wa afya kupitia mafunzo kwa wahudumu wa afya, kuimarisha mnyororo wa ugavi na kuboresha ufuatiliaji wa data.
• Muungano wa Kupeleka na Mawasilino ya Simu na Umeme Katika Vituo vya Afya: Kupitia mpango wa Power Africa, USAID inatarajia kutoa Dola za Kimarekani 600,000 kufanya kazi na makampuni binafsi yaliyo katika sekta ya mawasilino ya simu na teknolojia pamoja na Serikali ya Tanzania ili kupanua huduma za nishati safi na umeme katika zahanati na vituo vya afya 100 vilivyopo maeneo ya vijijini na miji midogo magharibi, kati na kusini mwa Tanzania. Zikitumia nishati safi, kampuni za mawasiliano ya simu zitajenga na kuimarisha huduma za data ili kuviwezesha vituo hivi kupata kwa uhakika na kutumia huduma muhimu za kidijitali. Matokeo yake ni kuwa vituo hivi vya afya vitaweza kuweka na kufuatilia kumbukumbu zake kwa uhakika; kutoa taarifa na kushughulikia matukio ya dharura kwa ufanisi; na kutoa ripoti mbalimbali kuhusu huduma zitolewazo kwa wagonjwa. Upatikanaji wa vyanzo safi na vinavyoaminika vya nishati, utaboresha utoaji wa huduma za msingi za afya na utawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata mwanga na nishati hivyo kuweza kuendesha shughuli zao za kila siku kwa ufanisi na tija.
•Usalama wa Afya Duniani: Kama sehemu ya jitihada za Serikali ya Marekani za kuhakikisha salama wa afya duniani (Global Health Security) na kusaidia kufikiwa kwa lengo ya Mkakati wa Kitaifa wa Kujilinda Dhidi ya Hatari za Kibaiolojia (National Biodefense Strategy) la kusaidia angalau nchi 50 kuboresha uwezo ulinzi wa kiafya, USAID na CDC, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo (Mwaka wa Fedha 2022-2024), zinapanga, kutoa takriban Dola za Kimarekani milioni 26 ili kuimarisha uwezo wa Tanzania kuzuia, kubaini na kukabiliana na milipuko ya maradhi ya kuambukiza. Bajeti ya Rais kwa Mwaka wa Fedha 2024 inajumuisha fedha za ziada kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 9 kwa ajili ya shughuli za USAID zitakazotolewa katika kipindi hicho cha miaka mitatu. USAID na CDC zitaimarisha ushirikiano wao na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto zinazokabili hospitali na vituo vya afya, wahudumu wa afya na wagonjwa kuzuia, kubaini na kushughulikia milipuko ya maradhi kwa kuimarisha maabara na uchunguzi/ufuatiliaji wa maradhi, ikiwemo maradhi yanayoambukiza wanyama na wanadamu (zoonotic diseases) kufuatilia usugu wa vimelea vya maradhi dhidi ya dawa (antimicrobial resistance); kuboresha udhibiti wa maambukizi; kuongeza uwezo wa kushughulikia kwa haraka milipuko ya maradhi. Aidha, USAID na CDC zitasaidia kuboresha usalama dhidi ya mambukizi ya vimelea vya kibaiolojia na kuhakikisha ulinzi dhidi ya hatari za kibaiolojia (biosafety and biosecurity); na kutoa taarifa za kuaminika kwa jamii kuhusu vitisho vya kuibuka kwa majanga ya maradhi na milipuko ya maradhi mengine ya kuambukiza nchini Tanzania.
• Msaada kukabili UVIKO -19: Tanzania ni mojawapo kati ya nchi 11 zilizo katika mpango wa kimataifa wa kupelekewa chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa wingi (Global VAX surge countries). Ubia kati ya Marekani na nchi hizo, ikiwa ni pamoja na ubia kupitia mpango wa Global VAX, umewezesha kupatikana matokeo makubwa sana. Kiwango cha utoaji chanjo kwa watu wanaostahili kupata chanjo hizo nchini Tanzania kiliongezeka sana kutoka asilimia 15 (mwezi Juni 2022) hadi asilimia 98.9 (ilipofika mwezi Disemba 2022). Kwa msaada wa mpango wa Global VAX, viongozi wa jamii waliwahamasisha watu kupata chanjo, na wahudumu wa afya walipita nyumba kwa nyumba kutoa chanjo katika maeneo magumu kufikika. # # #
No comments:
Post a Comment