HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 23, 2023

Kampeni ya Mikopo Kupitia Radio za Kijamii Yafanikiwa

HAKIKA kazi ya kuongeza uelewa kwa wananchi kupitia Radio za kijamii kumewanufaisha watanzania hasa kundi la watu wenye ulemavu kwa kupata taarifa sahihi kuhusu mkopo usiokuwa na riba ambapo taarifa hizo zilibadilisha maisha yao.

Kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma awamu ya pili (PS3+) kwa kushirikiana na TAMISEMI inahamasisha jamii, hasa wanawake, vijana na wenye ulemavu kuhusu uwepo wa mikopo ya asilimia 10.

PS3+ kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa pamoja wameweza kufanya kazi na Asasi za Kiraia mbalimbali watendaji kata, vijiji na mitaa kwa kuwahamasisha wananchi kuhusu uwepo wa mikopo ya asilimia 10 kwenye Halmashauri zao, namna wanavyoweza kupata mikopo hiyo ili kuweza kuboresha maisha yao na jinsi kurejesha mikopo hiyo.

Kabla ya ushirikiano huu, wananchi wengi kwenye maeneo yasiofikika kwa urahisi hawakufikiwa na hawakua na Uelewa mzuri juu ya mikopo ya asilimia 10 ndipo Ps3+ wakafadhili matangazo kwenye vituo vya Radio za Kijamii katika mikoa mbalimbali nchini ikishirikiana na TAMISEMI na Internews – Boresha Habari na hatimaye kupatikana matokeo chanya.

Programu hizi huongeza ufahamu wa mikopo, kueleza ni nani anayestahili mikopo hiyo na kutoa maelezo kuhusu jinsi ya kuipata.

Mhasibu wa shirika la watu wenye ulemavu la Nyota Njema mkoani Kigoma, Hakizimana Emmanuel alisema alisikia matangazo ya kipindi cha mkopo bila riba kupitia redio mkoani hapo ambapo awali hakuzipata taarifa hizo kwa usahihi kwa sababu alikuwa akisikia tetesi za kwamba matangazo yanapita barabarani kwa gari la matangazo.

Hakizimana alipopata taarifa sahihi shirika lao liliomba mkopo kupitia Ofisi ya Maendeleo ya Jamii.

Walipokea kiasi cha Shilingi milioni 10 ambazo walizitumia kupanua biashara yao iliyopo ya kutengeneza sabuni na kuanzisha biashara mpya ya usafirishaji wa sabuni mkoa jirani (Mwanza).

"Kwa mkopo huu tumebadilisha maisha yetu kama watu binafsi na kama jamii kifedha. Tuna uwezo wa kurejesha mkopo wetu kwa wakati na kupanua biashara yetu ya utengenezaji wa sabuni."

"Tunamiliki pikipiki mbili ambazo tunazitumia kusafirisha sabuni mkoani Mwanza.” alisema Hakizimana

Afisa Maendeleo ya Jamii Kigoma Ujiji, Jabiri Majira, alibaini kuongezeka kwa idadi ya maombi ya mikopo baada ya kampeni ya matangazo ya redio za jamii.

Alisema Katika robo tatu iliyopita, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii ilitoa zaidi ya milioni 260 (takriban Dola za Kimarekani 111,000) kwa vikundi zaidi ya 30 ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu ikilinganishwa na shilingi milioni 85 (takriban Dola 36,000) mwaka uliopita, ongezeko la zaidi ya asilimia 200. “Unaweza kuona jinsi watu wanavyochangamkia fursa hiyo ikilinganishwa na mwaka jana.

"Hili limefikiwa kupitia uhamasishaji unaofanywa na redio ya kibinafsi na ya jamii. Tunavishukuru sana redio hizi za kijamii za hapa nchini kwa kuwafahamisha watu kuhusu fursa zilizopo na tutaendelea kushirikiana nazo ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na ufahamu siku zote.” alisema Majira.

Mkurugenzi wa Tamisemi Dkt. Angelista Kihaga akizungumza na Michuzi Blog alieleza juu uelewa wa wananchi juu ya asilimia 10 ya mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu kutokana na kuongeza nguvu kwenye matangazo ya radio za jamii.

"Kwa sasa wananchi wana uelewa juu ya uwepo wa mikopo hii ya asilimia 10 kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuendelea kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali kama vile runinga, radio, mikutano na vikao kazi. Aidha, Halmashauri zote nchi zimeelekezwa kuhakikisha zinatoa tarifa kwa wananchi juu ya uwepo wa fursa za mikopo katika maeneo yao na pia kubandika matangazo ya kutoa mikopo kama ilivyoelekezwa katika sehemu ya 7(1) ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo ya mwaka 2019." Alisema Dkt. Kihaga.

Dkt. Kihaga alieeleza kabla ya mfumo huo kulikuwa na changamoto ya kutotolewa kikamilifu kwa mchango wa Halmashauri, mtu mmoja kukopa zaidi ya mara moja, na baadhi ya makundi kutorejesha mkopo.

"Baada ya maboresho ya Mfumo wa usimamizi wa mikopo wa asilimia 10 kupitia TPLMIS, mfumo umewezesha utambuzi wa wanufaika wa mikopo, usimamia marejesho ya mikopo upatikanaji wa taarifa sahihi za mikopo pia uwazi na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika usimamizi wa utoaji wa mikopo ya umeongezeka." Alisema.

Alisema mfuko huo unalenga kuwainua kiuchumi Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu.

Dkt. Kihaga alisema kuwa endapo mtu au kikundi hakijarejesha mkopo na endapo kikundi kitashindwa kurejesha mkopo baada ya muda wa nyongeza, mamlaka ya Serikali za Mitaa itatoa notisi kwa kikundi hicho kuhusu kusudio la kufungua shauri la madai dhidi ya wanakikundi kwa mujibu wa kanuni za utoaji mikopo za mwaka 2019.

Aliongeza kuwa endapo utafika muda wa kurejesha mkopo ambao ni baada ya miezi mitatu tangu siku ya kikundi kupata mkopo marejesho ya mkopo yatafanywa kila mwezi kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kati ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kikundi kilichopatiwa mkopo.

Aidha, bila kujali masharti ya sehemu ya 11 kanuni ndogo ya (1) na (2) mamlaka ya Serikali ya Mtaa inaweza kuingia makubaliano na kikundi kilichopatiwa mkopo kuhusu namna bora zaidi ya urejeshaji wa mkopo huo.

Akielezea utaratibu wa kupata mkopo Dkt. Kihaga alisema kikundi baada ya kuomba mkopo watalazimika kuingia katika mfumo wa usajili na kuomba mkopo kupitia tovuti ya Mkopo wa Tamisemi wakiwa na kitambulisho cha NIDA, kikundi kitaingiza taarifa za wanachama wake na tarifa za kikundi katika mfumo kwaajili ya kupata cheti cha utambuzi.

Baada ya kupata cheti cha utambuzi, mfumo utakiruhusu kikundi hicho kuomba mkopo.
Akizimana Emmanuel mwenye tisheti nyeupe na mwenzake, ambao ni wanachama wa Kiwanda cha Sabuni cha Kikundi cha Walemavu cha Nyota Njema kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma wakionyesha aina ya sabuni wanazotengeneza kiwandani hapo kufuatia kunufaika na mkopo usio na riba.
Elias Muhonyi Mwanachama kutoka kikundi cha walemavu cha Ruchungi kutoka Halmashauri ya Uvinza mkoani Kigoma, akimuhudumia mtoto kutokana na biashara aliyoianzisha baada ya kunufaika na mkopo usio na riba
Wanachama wa kikundi cha walemavu cha  Ruchungi cha Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Mwanachama wa kikundi cha walemavu cha Ruchungi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Kigoma akionyesha biashara yake ya kushona viatu aliyoanzisha baada ya kunufaika na mkopo usio na riba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad