HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 7, 2022

UBORESHAJI WA MITAALA NA SERA YA ELIMU YA MAFUNZO KUIMARISHA ELIMU NCHINI-PROF MKENDA

 Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kwa sasa mageuzi ya elimu yanafanyika dunia nzima na kueleza kuwa zoezi la maboresho ya mitaala na sera ya elimu na mafunzo linaendelea hapa nchini limelenga kuimarisha elimu na kuifanya isaidie jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema hayo akifungua Mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma ukiwahusisha wadau mbalimbali kutoka katika sekta ya elimu nchini alisema maboresho hayo yana lengo la kuwa na elimu yenye ubora na itakayomwezesha mwanafunzi kuwa na ujuzi, maarifa na uwezo wa kuweza kujitegemea, kujiajiri na kuajiriwa..

Mkutano huo siku mbili unahudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Unesco,Kamati ya Kitaifa ya Maboresho ya Mitaala inayoongozwa na Prof. Makenya Maboko, wajumbe pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba una lengo la kujadili maendeleo ya elimu nchini.

“Mageuzi ya elimu kwa sasa yako dunia nzima na sisi hapa nchini tunaendelea na zoezi la maboresho ya mitaala na sera lenye lengo la kuwa na elimu yenye ujuzi kwa wanafunzi wajitegemee na kuongeza ubora wa elimu nchini” amesema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael amewataka washiriki wa mkutano huo kuwa na majadiliano ya elimu yenye tija na yenye kuleta mabadiliko kwenye elimu nchini.

Alisema mkutano huo utatoka na mawazo ya kuboresha elimu nchini na na kuangalia namna ya uboreshaji wa elimu katika hatua mbalimbali.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maboresho ya Mitaala Prof. Maboko anatarajia kupata nafasi ya kueleza mkutano huo maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa katika zoezi linaloendelea la kuboresha mitaala ya elimu hapa nchini.

Awali akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo nchini, Mkuu wa kitengo cha Elimu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Faith Shayo, alisema wamefurahishwa sana na namna ambavyo serikali ya awamu ya sita inavyojikita zaidi katika masuala ya elimu ili kuwezesha watanzania kujiajiri, kuajirika na kuajiri wengine.

Alisema wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu wanauona umakini wa serikali katika kubadili sekta ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae.

Alisema kutokana na mabadiliko hayo, mengi mazuri yamekuwa yakijitokeza ikiwamo ya kuandikishwa kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za msingi kwa taarifa ya mwaka 2021, ambapo mwaka 2020 kulikuwa na wanafunzi 11,196,788 ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na wanafunzi 8,363,386 huku idadi ya wanaomaliza darasa la saba ikiongezeka kwa asilimia 81 kwa mwaka 2020 kutoka asilimia 67 za mwaka 2015.

Aidha ufaulu uliongezeka kwa asilimia 82 kwa mwaka 2020 kutoa asilimia 57 kwa mwaka 2015.

Shayo aliishukuru sana serikali kwa kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na ya wazi na wadau wa elimu ikiwemo sekta binafsi kuona namna bora ya kuimarisha elimu nchini Tanzania ili wahitimu waweze kujiajiri au kuwa na uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.

Alitaka washiriki wa mkutano huo kuchambua kwa makini taarifa zilizopo na kuweka wazi majibu yake kwa manufaa ya taifa.

Alisema katika mkutano wa kimataifa Septemba mwaka huu huko New York kuhusu elimu katika dunia iliyoitishwa na Covid 19 Tanzania iliahidi kufanya mabadiliko katika mfumo wake wa elimu ili kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma kama ilivyoelekezwa na agenda 2030, hivyo ni matumaini yake kwamba wajumbe watajadili changamoto za elimu na kuzipatia majawabu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akifungua mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael akizungumza wakati wa mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Mkuu wa kitengo cha Elimu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Faith Shayo akitoa salamu za wadau wa maendeleo katika sekta ya elimu wakati wa mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akitoa salamu za kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo wakati wa mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Bw. Michel Toto akifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maboresho ya Mitaala, Dkt. Jenifer Sesabo pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maboresho ya Mitaala Prof. Makenya Maboko wakati wa mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Pichani juu na chini ni wadau wa sekta ya elimu kutoka balozi, taasisi mbalimbali za sekta binafsi na serikali pamoja wanafunzi walioshiriki katika mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.
Pichani juu na chini ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu nchini walioshiriki mkutano wa mwaka 2021/2022 wa wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini unaofanyika Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Tume ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad